26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

JK alaani mauaji ya albino

jakayaNa Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete amesema anasikitishwa na kitendo kilichoibuka upya cha mauaji ya albino baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011.
Amesema kutokana na hali hiyo amekubali kukutana na viongozi wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi nchini (Albino), ili kuweza kusikiliza maoni yao juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hilo.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, ambapo alisema ni lazima jamii ilaani vikali mauaji dhidi ya albino kwani mauaji ya kinyama hayakubaliki.
“Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi. Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hili.
“Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yoyote ya watu waliostaarabika ya watu wanaomwabudu Mungu. Watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wengine.
“Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa. Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao. Jamii nzima na sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo kwa watu wengine wote,” alisema Rais Kikwete.
Alisema anaamini ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii utawezesha kutokomeza mauaji ya albino na kuliondolea taifa aibu.
Rais Kikwete alisema mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa na kwamba ni vitendo visivyovumilika.
Alisema Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa hai.

DARUSO
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) imelaani mauaji na vitendo vya kikatili wanavyotendewa albino kila inapofika wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Habari na Mawasiliano (DARUSO), Jalia Yahaya, alisema mauaji hayo yameonekana kuwa ni janga kwa kuwa yanajirudia rudia kila mara.
Alisema imani potofu, ujinga na uvivu ndiyo sababu kubwa zinazowafanya watu kuwatendea albino ukatili huo.

HALI YA USALAMA
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete akizungumzia kuhusu usalama hapa nchini, alisema kwa ujumla hali ni nzuri, lakini kuna matukio ya kiusalama ambayo yana sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi.
Alisema matukio hayo yana sura mbili, ikiwamo ujambazi na mengine yenye dalili za ugaidi.
Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miezi 12 hivi kumekuwa na matukio ya watu kuvamia vituo vya polisi, wengine wanachoma moto au wengine wanapora silaha.
“Pia kumekuwapo na matukio ya kuwashambulia polisi walioko kwenye doria na wengine kuporwa silaha. Vituo vya polisi vilivyovamiwa na silaha kuporwa ni vya Newala mkoani Mtwara ambako silaha tatu ziliporwa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji silaha saba, Kimanzichana, Mkuranga silaha tano, mbili za polisi na tatu za raia waliokwenda kuzihifadhi pale, na Ushirombo, Wilaya ya Bukombe silaha 18.
“Pugu Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa silaha tatu. Kule Songea kulikuwapo na matukio mawili ya polisi kushambuliwa, lakini silaha hazikuporwa.
“Bahati mbaya, vijana wetu saba wa Jeshi la Polisi walipoteza maisha katika matukio hayo. Newala alikufa polisi mmoja, Kimanzichana mmoja, Ikwiriri wawili, na Ushirombo watatu. Wapo polisi kadhaa waliopata majeraha ya namna mbalimbali katika mashambulizi haya,” alisema.
Alisema pamoja na hali hiyo, silaha zote 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa.

KURA YA MAONI
Akizungumzia kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, Rais Kikwete, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa maelekezo husika kuhusu kampeni wakati ukiwadia.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba Watanzania wawe na subira na kuzingatia masharti ya sheria ya kura ya maoni na kanuni zake.
“Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu. Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa, amani na usalama,” alisema.

UANDIKISHAJI BVR
Akizungumzia uandikishaji wapigakura kwa kutumia mashine za BVR, alisema unaendelea vizuri kwani idadi ya waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa kipindi kilichopangwa katika kata husika.
Alisema pamoja na changamoto hizo, zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji wa wapigakura.
“Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la uboreshaji wa daftari na uandikishaji wa wapigakura limeanza vizuri Makambako. Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa. Kati ya Februari 23 hadi 25 NEC ilitegemea kuandikisha wapigakura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi kuwa mkubwa wameweza kuandikisha wapigakura 13,042.
“Kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapigakura 80 na 150 kwa siku. Lengo la tume ni kuandikisha wapigakura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles