27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Rais, mtangulizi wake hawaivi Botswana

GABORONE, BOTSWAN



KATIKA hatua isiyo ya kawaida, Rais Mokgweetsi Masisi ametumia hotuba yake ya kwanza ya hali ya taifa (SONA) kumshambulia hadharani mtangulizi wake, Rais mstaafu Ian Khama.

Masisi ambaye aliteuliwa na Khama, aliingia madarakani Aprili mwaka huu wakati mtangulizi wake huyo alipong’atuka baada ya kutumikia miaka 10 madarakani.

Lakini wawili hao tangu hapo wamekuwa hawaivi wakishambuliana hadharani na kutishia ustawi na uimara wa Serikali.

Akitoa hotuba hiyo bungeni juzi, Masisi alisema; “Raia wa Botswana wote wanatambua uhamishaji madaraka kutoka utawala uliopita haujawa mzuri kama ilivyotarajiwa.

“Hata hivyo inapaswa ieleweke kuwa nimejaribu kufanya kila linalowezekana kurahisisha mchakato huo kwa kutumia raia waandamizi kama vile; Mheshimiwa Rais mstaafu Dk. Festus Mogae, Mheshimiwa Dk. Ponatshego Kedikilwe, Mheshimiwa Ray Molomo, Mheshimiwa Patrick Balopi na Mheshimiwa David Magang kusaidia uhamiaji mzuri wa madaraka.

“Lakini ninasikitika kutangaza juhudi hizo hazijazaa matunda kufikia sasa. Katika utamaduni wa kweli wa Botswana, usuluhishi wa aina hiyo unapaswa kuendelezwa kwa faida ya kila mtu.”

Ofisi ya Khama haikuweza kupatikana mara moja kuzungumzia kauli hiyo ya rais.

Hata hivyo, Khama (65) ameripotiwa kukasirishwa na kinachodaiwa hatua ya Masisi (57) kumkatalia kutumia ndege za Serikali huku vyombo vya habari vya umma vikiagizwa kutotangaza habari zake.

Wawili hao pia wametofautiana kuhusu bosi wa zamani wa Kurugenzi ya Usalama na Intelijensia  (DIS), Isaac Kgosi, ambaye alifukuzwa na Masisi kwa kukosa utii.

Baada ya Kgosi kutimuliwa, Khama aliamua kumwajiri kuwa katibu wake binafsi hatua inayodaiwa kuzuiwa na Masisi.

Masisi alitumikia kama makamu wa rais wa Khama na alimrithi miezi 18 kabla ya uchaguzi wa wabunge utakaofanyika mwakani.

Wawili hao ni wakongwe wa chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP), kilichopo madarakani tangu uhuru kutoka Uingereza mwaka 1966.

Baba wa Khama, Seretse Khama alitumikia kama rais wa kwanza wa Botswana 1966 hadi 1980.

Botswana inafahamika duniani kwa kiwango kidogo cha rushwa, utawala bora na sheria na inahesabiwa kama simulizi ya mafanikio barani Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles