30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi: bado hatujawanasa watekaji wa MO

Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAA



JESHI la Polisi  limesema linaendelea kuwafutilia watu waliohusika kumteka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji(MO) waweze kuchukuliwa hatua za sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Liberatus Sabas alisema watawafuatilia popote walipo na wakibainika watawachukulia hatua za sheria ikiwamo kuwafikisha mahakamani kwa utekaji.

“Bado tunaendelea kuwasaka wahusika hao, tutawafuatilia popote walipo  tuweze kuwakamata na kuwafikisha mahakamani kwa ajili ya hatua nyingine za sheria kwa sababu ni wahalifu kama walivyo wahalifu wengine,”alisema Sabas.

Alisema hakuna kisichowezekana katika kazi zao hivyo anaamini watapatikana kama walivyofanikiwa kumpata mfanyabiashara huyo siku chache baada ya kutekwa na watu hao.

“Kwa sababu uchunguzi unaweza kuchukua muda mrefu, lakini tunaamini tutawapata kama Mo mwenyewe tulivyompata na tutatoa taarifa kama tulivyoahidi   baada ya kuwakamata  wananchi waweze kuwajua,”alisema.

Mo Dewji alitekwa Oktoba 11 akiwa anaingia kwenye jengo la Colleseum asubuhi na watekaji waliotajwa kwamba ni raia wa kigeni ambao hawajakamatwa.

Akizungumzia kuhusiana na vigogo wa Kampuni ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Mkoa wa Dar es Salaam, Uda-Rapid Transit (UDART), Kamanda Sabas alisema   suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi licha ya yeye kutokuwa na taarifa za kina.

“Mimi nimekaimu nafasi hii, sina taarifa za kina kuhusiana na suala hilo ila naamini kama lipo hapa linaendelea kufanyiwa kazi,”alisema.

Vigogo hao akiwamo wa idara ya fedha kwa pamoja wanatuhumiwa kuhusika katika mtandao wa uhujumu wa mapato ya mabasi ya mwendokasi kwa kuchapisha tiketi feki kwa abiria.

Kamanda Sabas alisema katika operesheni za kawaida, jeshi hilo linawashikilia watu 15 akiwamo Dk. Yusuph Mwaipopo wakidaiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa magari.

Alisema watu hao   walikamatwa juzi baada ya kufanyika  operesheni ambayo pia ilisaidia kupata magari 15 yaliyoibwa katika maeneo mbalimbali.

“Miongoni mwa magari yaliyoibwa ni pamoja na gari la Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambalo liliibwa maeneo ya Mbagala na kukamatwa Mikumi mkoani Morogoro likiwa linasafirishwa kupelekwa  mikoa mingine ya nchi,”alisema.

Alisema gari jingine lililokamatwa kwenye operesheni hiyo ni llinalomilikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa CCM  (UWT) ambalo liliibwa Mbagala hivi karibuni.

Alisema jeshi hilo bado linaendelea na mahojiano na watu hao   kubaini mtandao mzima wa wizi wa magari na kuwachukulia hatua za sheria.

Kamanda Sabas alisema  kuna magari mengine manne yalioibwa mkoani humo yanarudishwa kwa ajili ya utambuzi.

Alisema mkakati wa jeshi ni kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya wizi wa aina yoyote  wananchi waweze kuishi kwa usalama bila wasiwasi wowote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles