RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuongoza mamia ya waombolezaji katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa mwasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, wakati akizungumza na MTANZANIA, ambapo alisema mwanasiasa huyo mkongwe atazikwa katika makaburi ya familia kijijini kwao Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Alisema kuwa Rais Kikwete anatarajia kuongoza umati wa Watanzania pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na wa vyama vingine vya siasa katika ibada ya mazishi itakayo fanyika kijijini humo.
Aidha alisema kabla ya mwili huo kupelekwa kijijini kwao utaagwa nyumbani kwake shanty town Moshi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini (KKKT) Shanty Town saa sita mchana na kisha kuanza safari kuelekea kijijini kwao Usangi.
Gama alisema baada ya mwili huo kuwasili kijijini kwao ibada ya mazishi na shughuli zote za mazishi ikiwemo salamu za rambirambi zitaanza majira ya saa tatu asubuhi.
“Mazishi ya marehemu Peter Kisumo yanatarajiwa kuhudhuriwa na mheshiwa Rais Kikwete pamoja na viongozi mbalimbali wa kisiasa na kiserikali, kabla ya kuusafirisha mwili wake tutaanza kuuaga leo katika kanisa la KKKT shant Town”alisema Gama.
Alisema marehemu Peter Kisumo aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ambapo aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa miongo miwili, mwasisi wa CCM pamoja na mdhamini wa chama hicho.