SERIKALI mkoani Tanga imeliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi ya wilaya, kuhakikisha wanakomesha migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo imechangia kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Magalula Said Magalua wakati wa hafla ya kumsimika kiongozi mkuu wa wafugaji, Lweigwanani iliyofanyika katika Kijiji cha Elerai kilichopo Kata ya Kibrashi wilayani humo.
Alisema endapo viongozi hao watashirikiana kwa pamoja wataweza kuzuia au kukomesha kabisa mapigano ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji ambayo yanasababisha baadhi ya watu kuuawa.
“Niwaombea pangeni timu za kuhakikisha mnashirikiana kati ya watendaji wa serikali, jeshi la polisi pamoja na hawa viongozi wa kimila ambao ndio wakuu wa jamii za wafugaji ili kutafuta namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi katika wilaya hii,” alisema RC Magalula.