28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kikwete azindua meli za vita Dar

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam
AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, amezindua na kuidhinisha rasmi matumizi ya meli mbili za vita ambazo ni P 77 Mwitongo na P 78 Msoga na kusema huo ni mwanzo wa kutokomeza uharamia na wizi wa rasilimali katika eneo la Bahari ya Hindi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa meli hizo jana katika kambi ya Jeshi la Wanamaji (NAVY), iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema zimepatikana wakati mwafaka ambapo taifa linahitaji ulinzi katika eneo la bahari kufuatia uzalishaji wa gesi na mafuta.
“Kumekuwapo na uharamia na wizi katika eneo la bahari yetu, lakini meli zetu tulizonazo hazina uwezo wa kufika bahari ya kina kirefu. Tumekuwa tukishirikiana na Jeshi la Afrika Kusini katika kufanya doria kwenye mipaka ya bahari, lakini kuanzia leo tutatumia meli zetu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kabla hajaondoka madarakani atahakikisha jeshi hilo linapata meli nyingine ikiwa ni lengo la kukamilisha mpango wa miaka 15 wa kuimarisha Jeshi la Wananchi.
Pamoja na hatua hiyo, pia Rais Kikwete aliipongeza Serikali ya China pamoja na kampuni iliyounda meli hizo ya Poly Technologies Inc ya nchi hiyo.
“Katika maendeleo ya jeshi la Tanzania hakuna mshirika wa kufananishwa na Jamuhuri ya watu wa China kwa mchango wao mkubwa,” alisema .
Naye Balozi wa China hapa nchini, Dk. Lu Youqing, alisema ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi hizo mbili na kwamba utaendelea kudumu ili kuwaenzi waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung.
Awali akizunguzia uzinduzi wa meli hizo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ), Jenerali Devis Mwamunyange, alisema meli hizo zimepewa majina ya vijiji walikozaliwa viongozi wa taifa kikiwamo kijiji cha Mwitongo alikozaliwa Mwalimu Nyerere na Kijiji cha Msoga ambapo amezaliwa Rais Kikwete kama hatua ya kuenzi mchango wao kwa taifa.
Akielezea sifa za meli hizo, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Meja Jenerali Rogasian Laswai, alisema zina urefu wa mita 60 na zimesheheni silaha nzito za kivita ikiwamo mizinga mikubwa na midogo yenye uwezo wa kupiga umbali wa kilometa tisa kwenda mbele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles