23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Escrow yampa tuzo Kafulila

david KAFULILANa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amekabidhiwa tuzo ya utetezi bora wa haki za binadamu kwa mwaka 2015 kama njia ya kutambua mchango wake kwa kutetea jamii.
Mbali na Kafulila wengine waliopewa tuzo hiyo ya heshima ni mwandishi wa habari wa gazeti Mwananchi, Salma Said Hamoud na mwanaharakati kutoka wilayani Ngorongoro katika Kijiji cha Loliondo, Maanda Ngotika.
Tuzo hizo walikabidhiwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Bindamu, Bennedict Alex, katika maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu ambayo hufanyika Aprili 28 ya kila mwaka na kuandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Kafulila alipewa tuzo hiyo kutokana na msimamo wake juu ya hoja ya ufisadi wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambapo zaidi ya Sh bilioni 300 zilibainika kuchotwa.
Mbunge huyo alisimama kidete kutetea hoja hiyo licha ya baadhi ya viongozi wa Serikali kujaribu kuizima.
Akieleza hatua hiyo pamoja na kumtambua, Mwenyekiti wa Bodi ya THRDC, Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema Kafulila ni mbunge ambaye alithubutu kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya kutetea masilahi ya taifa na watu wake.
“Ikumbukwe kwamba mbunge huyu alikumbana na kila aina ya vitisho wakati wa hoja hii, hata hivyo pamoja na hoja yake kujaribu kuzimwa mara tatu ndani ya Bunge bado aliendelea kusimamia ukweli hadi pale ilipokuja kudhihirika na wahusika kuchukuliwa hatua,” alisema Dk. Bisimba.
Kwa upande wa mwandishi wa habari, Salma, alipewa tuzo hiyo kwa kusimamia hoja yake ya kutetea masilahi ya Zanzibar kwa kuitambua kama nchi ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ambapo naye alikuwa ni mmoja wa wajumbe kutoka visiwani Zanzibar.
Msimamo wake umeelezwa ulimfanya mwanahabari huyo kupokea kila aina ya vitisho hali iliyomfanya atumie njia za panya kutoroka mjini Dodoma na kufika jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa mshindi mwingine wa tuzo hiyo, Ngotika, ilielezwa kuwa ni mmoja wa wanaharakati ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipambana kuzuia kuondolewa kwa wakazi wa Loliondo na ardhi yao kupewa mwekezaji.
Kutokana na mapambano hayo, Ngotika aliwahi kupelekwa polisi na hata kusingiziwa kuwa ni raia wa Kenya kama mbinu za kumfanya ashindwe kuendelea kuwatetea wananchi wa Loliondo.
Akieleza lengo la maadhimisho hayo, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema yamelenga kuthamini, kutambua na kuwaleta pamoja watetezi wa haki za binadamu nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles