30.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Brigedia Jenerali Mbita kuzikwa leo

mbitaAdam Mkwepu na Easther Mnyika, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Brigedia Jenerali mstaafu Hashim Mbita (82), anatarajiwa kuzikwa leo jijini Dar es Salaam.
Mbita aliyefariki dunia Mei 26, mwaka huu katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, anatarajiwa kuzikwa leo alasiri katika makaburi ya Kisutu.
Kifo cha mpigania uhuru huyo wa nchi za Afrika kimewagusa viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali ambapo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, akisema atakumbukwa kwa kusimamia misingi ya uadilifu na kujituma.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Chang’ombe jijini Dar es Salaam jana, Kinana alisema suala la kujituma ilikuwa ni moja ya nguzo ya Brigedia Jenerali Mbita wakati wote wa uhai wake.
“Inasikitisha sana kuona suala hili wanaachiwa wanasiasa peke yake na jamii ikijitenga wakati hili ni letu wote na litaanza kwa kuenzi na kudumisha mazuri yaliyofanywa na wakombozi akiwemo marehemu Hashimu Mbita,” alisema Kinana.
Alisema kabla ya kuwa katika kamati ya ukombozi, alikuwa mwanaharakati shupavu wa siasa kutokana na vyeo mbalimbali alivyopitia kuanzia mwaka 1970 hadi 1972 ikiwamo kuwa mwandishi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Kinana alisema kutokana na uadilifu na uaminifu wa kiongozi huyo, aliweza kudumu katika Baraza la Ukombozi la nchi za Afrika kwa zaidi ya miaka 20 na hata baada ya kustaafu alipewa jukumu la kuandika taarifa ya shughuli zote za ukombozi alizofanya.
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alisema alimfahamu Mbita tangu akiwa mwandishi na mwanasiasa.
“Mbita alikuwa shupavu, hodari, mpenda nchi, kazi na mwenye kujitoa. Pia alikuwa na imani katika majukumu yake, hivyo tumempoteza kiongozi wa kipekee,” alisema Mkapa.
Alisema kutokana na umahiri wake, kuna kitabu kitazinduliwa hivi karibuni ambapo kitaelezea historia yake kwa ujumla.
Kutokana na hilo, Mkapa alitoa wito kwa vijana kumuenzi marehemu Mbita kwa mazuri.
Kitabu cha Mbita kilichopewa jina la “Mradi wa Hashim Mbita” kimeratibiwa na viongozi wa nchi za SADC katika kuthamini harakati za ukombozi na juhudi zilizotukuka za kiongozi huyo mahiri Afrika.
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombare Mwiru, alisema ukimuondoa Mwalimu Nyerere, Rashid Kawawa, Thabiti Kombo na Abeid Karume anayefuata kwa heshima ni Hashim Mbita.
“Mbita alikuwa hodari wa kuratibu na kuunganisha watu na pia alijua kufanya kazi na vilevile alitoa mchango katika chama cha TANU,” alisema Kingunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles