26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Rais anapodai Mungu amemwambia aache kutukana  

rais-rodrigo-dutetreMAFUNDISHO ya imani mbalimbali duniani yanasema Mungu huwasiliana na wanadamu kwa namna mbalimbali zinazobadilika kila mara, tangu zama za manabii waliofikisha ujumbe wake unaoasa kutimiza matakwa yake ili kuepuka ghadhabu yake, lakini inavyoelekea sasa Mungu haongei na manabii pekee bali na yEyote anayemchagua.

Rais Rodrigo Dutetre wa Philippines anayefahamika kwa kauli tata za kutukana viongozi wenzake wa kisiasa duniani, ambaye tangu aingie madarakani katika taifa hilo ameweka historia ya kutatua matatizo ya nchi hiyo kwa njia ya mkato bila kujali sheria, hivi karibuni alitoa unabii wa mazungumzo yake na Mungu kwa mujibu wa madai yake.

 Kama ni Mungu aliongea naye au ufahamu wake au shetani ni vigumu kuthibitisha kwani Rais Dutetre amewahi kumwita Rais Obama wa Marekani mtoto wa kahaba, akamshambulia Papa Francis kutokana na kiongozi huyo wa Wakatoliki duniani kusababisha msongamano wa magari nchini mwake alipotembelea taifa hilo.

Akamtusi balozi wa Marekani nchini mwake kuwa ‘shoga’ na Katibu Mkuu wa UN aliyemaliza muda wake, Ban Ki Moon kuwa mwanajopo la wanaharamu wasiofaa.  Alikerwa na Katibu huyo wa UN aliyemshutumu kwa mauaji ya raia wake katika kampeni ya kupambana na magenge ya wahalifu wakiwamo wauza madawa ya kulevya iliyosababisha vifo vya raia 1,800 kwa kutotenganisha wahusika na wasiohusika.

Rais huyo mtata alianza kauli zake za kuudhi katika kampeni zilizomuingiza madarakani, alipotamka jukwaani kuwa mauaji na ubakaji ya mwaka 1989 ulichochewa na urembo wa waathirika, kwamba akiwa Meya wa Manila alipaswa kuwa wa kwanza kubaka kutokana na uzuri wa kuvutia na hakuwahi kuomba radhi kwa  matamshi hayo.

Katika hatua isiyotarajiwa Rais huyo aliwaita waandishi wa habari mnamo siku sita zilizopita na kuwapa ufunuo wake, kwamba akiwa katika moja ya safari zake za kikazi akitumia usafiri wa ndege Mungu aliongea naye na kumwambia aache tabia yake ya kutukana ovyo na asipoahidi kutimiza hilo Mungu ataiangusha ndege hiyo na kumuua.

 Kwa mujibu wa Rais Dutetre aliuliza sauti aliyoisikia ni ya nani? Alijibiwa kuwa ni Mungu hivyo akamuahidi kuwa atatimiza agizo lake kwa kuacha matusi, kwamba ahadi aliyoitoa kwa Mungu ni ahadi kwa wananchi wote nchini mwake japokuwa kama ni kweli aliongea na Mungu au atazingatia ahadi yake ni suala lingine, kwani katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema kuwa yeye ni binadamu wa kawaida kama wengine mwenye udhaifu wake, hivyo anaweza kuingia majaribuni na kushindwa kutimiza alivyoahidi kwa Mungu.

Lakini Rais huyo aliyeingia madarakani miezi mitano iliyopita baada ya kushinda uchaguzi alishaashiria hulka ya sera zake wakati wa kampeni, alipounga mkono mauaji ya wauzaji na watumia ‘unga’ bila kufuata taratibu za kisheria, akiunga mkono makundi ya wanamgambo yaliyowashughulikia wahalifu hao na kuwajumuisha wasio na hatia wakiwamo watoto wa mitaani. ‘Nabii’ Dutetre aliyekanywa na Mungu asitukane na abadili tabia alimshinda mpinzani wake wa karibu kwenye uchaguzi, Mar Roxas kwa kujizoelea kura milioni 16, 601, 997 na kutangaza sera ya kuisafisha nchi yake dhidi ya magenge ya wauza unga.

 Aliposhutumiwa na UN kwa mauaji katika kampeni yake ya ‘safisha Ufilipino’ alitishia kuiondoa nchi yake katika uanachama wa umoja wa mataifa na kuunda umoja mpya na China na mataifa ya Afrika. Akajinadi kuwa taifa lake litafuata sera za siasa huru zisizoingiliwa na mataifa ya nje kwenye uamuzi wa masuala yanayoihusu nchi hiyo, lakini tofauti na anavyotazamwa na mataifa duniani kutokana na hulka yake Rais huyo mbabe anapendwa nchini mwake kama maoni yaliyokusanywa na watafiti wa takwimu yalivyobainisha, alijizolea asilimia 91 ya kukubalika kwa staili yake ya uongozi na ndiye kiongozi aliyepata kuhusudiwa zaidi nchini humo kuliko kiongozi yoyote katika miaka ya hivi karibuni.

Huyu ndiye Rais wa pili mwenye umri mkubwa kutawala nchi hiyo akiwa na miaka 71 baada ya Rais wa zamani Sergio Osmena, lakini pia ndiye Rais aliyethubutu kufumbia macho historia mbaya ya mauaji na udikteta wa Rais wa zamani Hayati Ferdinand Marcos, anayekumbukwa na Wafilipino kwa utawala wake wa miongo miwili uliogubikwa mauaji ya kikatili. Dutetre aliruhusu mwili wa Dikteta huyo wa zamani kuzikwa katika makaburi ya mashujaa kwani alikuwa Rais na askari aliyepigania taifa lake, hatua iliyowakera wananchi wake wanaokumbuka ukatili wa Hayati Marcos.

 Sifa nyingine ya serikali ya sasa chini ya uongozi wa Rais Dutetre ni kutozuia uhuru wa habari lakini pia hajali sana usalama wao, kwani ana mtazamo tofauti kuhusu mauaji ya waandishi nchini mwake ambapo idadi kubwa ya waandishi wameuawa tangu wakati wa utawala wa Marcos. Amewahi kukaririwa akidai kuwa: “wengi kati ya waandishi waliouawa wamejisababishia wenyewe hatima yao, huwezi kuuawa kama hujafanya jambo lolote baya na kama wewe ni mwandishi kanjanja mpenda mshiko, lazima utauawa maana ni mwanaharamu”. Huyo ndiye ‘Nabii’ Rais Dutetre wa Ufilipino mwenye hulka tata inayompa umaarufu duniani. 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles