24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

FBI yatikisa mbio za urais Marekani

trump-hilary* Yampa nguvu Trump, yamwadhiri Hilary

Na JOSEPH HIZA

KITENDO cha Shirika la Upelelezi Marekani (FBI) kutangaza kubaini barua pepe mpya zinazoweza kuwa muhimu kwa uchunguzi dhidi ya mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton kumezitikisa mbio za kuelekea White House.

Uamuzi huo usiotarajiwa ulifanywa Ijumaa iliyopita na Mkurugenzi Mkuu wa FBI, James Comey huku akifahamu fika unaweza kushawishi matokeo ya uchaguzi kipindi hiki, ambacho ni siku chache tu kabla ya upigaji kura kimeshutumiwa na wengi.

Si tu na wanachama wa Democratic bali pia wale wa Chama cha Republican, ambacho mgombea wake ni bilionea, Donald Trump.

Democrat wana wasiwasi ugunduzi huo mpya unaweza kumpa nguvu mgombea wa Republican katika wiki ya mwisho kuelekea uchaguzi wa rais Novemba 8 mwaka huu pamoja na kuwaongezea nguvu wagombea wa useneta na baraza la wawakilishi.

Katika hatua tofauti kufuatia kadhia hiyo, Mwanasheria Mkuu wa zamani Eric Holder na waendesha mashitaka wengine kadhaa wametia saini barua inayomkosoa Comey kwa uamuzi wake huo, ambao unaaminika kuwa chanzo cha kubadilika ghafla kwa mwelekeo wa kura za maoni hadi sasa.

Kabla ya tangazo lake hilo Clinton alikuwa akiongoza kwa pengo la pointi 12 dhidi ya mpinzani wake huyo, lakini sasa limekuwa likipungua kwa kasi hadi kufikia pointi moja.

Aidha wafuasi wa Clinton wanamtuhumu Comey, ambaye ni mfuasi wa Republican kushawishiwa kisiasa kwa kumuandama Clinton.

Mkuu wa Kampeni za Clinton, John Podesta anasema Comey anaeneza dhana bila ya kuwa na ushahidi wowote kwa malengo anayojua yeye mwenyewe.

Kadhia hiyo inahusiana na madai kuwa Clinton alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, alitumia kompyuta yake binafsi kuandika pia risala za kikazi.

Aidha Katika barua yake kwa Comey, kiongozi wa kundi la wachache katika Baraza la Seneta, Seneta Harry Reid wa Jimbo la Nevada alimtumumu bosi huyo wa FBI kwa undumilakuwili.

Reid alikumbushia wito wa Democrat kujadili kile kinachoelezwa uwezekano wa uhusiano baina ya Trump na Serikali ya Urusi, tuhuma ambazo Comey alionekana kuzipuuza.

Badala ya Coney bila kutarajiwa akaja kuibua suala hilo jipya pamoja na sakata la ujumbe wa ngono unaotokana na uchunguzi dhidi ya Anthony Weiner, mbunge wa zamani wa New York na mume wa zamani wa msaidizi mkuu wa Clinton, Huma Abdidin.

Katika taarifa hiyo Reid amemwambia kiongozi huyo kuwa na jitihada za wazi kabisa zenye kuonesha ana nia ya kusaidia upande mmoja wa chama ushinde uchaguzi huo.

Aidha ameongeza kuwa ofisi yake imemwandikia barua hiyo kwa kutanabaisha kuwa amekiuka sheria iitwayo ‘Hatch Act’, ambayo inawazuia maafisa wa FBI kutumia mamlaka yao kufanikisha ushawishi katika chaguzi.

Amesema kwa kitendo cha kujiegemeza kwa upande wa chama amevunja sheria za taifa hilo.

Wakati suala hilo likionekana kumwathiri Clinton kwa vile ndilo linalozungumzwa zaidi kwa sasa na kufifisha ile kashfa ya kudhalilisha wanawake kingono iliyokuwa ikimwandama Trump, mpinzani wake huyo anaonekana kupata nguvu mpya, akithubutu kushambulia hadi katika majimbo yanayojulikana kuwa ngome za Democratic.

Katika kampeni zake za sasa anarudia kauli zake za mara kwa mara kuwa Clinton ni familia ya kihalifu na inastahili kuwa jela huku akipongeza FBI kwa kufichua sakata jipya.

Awali Trump alilia na FBI wakati ilipotangaza kutomshitaki Clinton kutokana na uzembe wa kutumia barua pepe binafsi kwa masuala nyeti ya kitaifa miezi michache iliyopita.

Kutokana na hali hiyo Clinton yu katika changamoto na anatakiwa kujiwekea mikakati ili kuhakikisha ndoto yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais Marekani inabakia pale pale. Inaweza kuwa pamoja na;

Kudai maelezo zaidi kutoka kwa Comey

Huu ulikuwa mkakati wa mwanzo wa Clinton wakati wa mkutano wake na wanahabari Ijumaa iliyopita, ambapo alisikika akisema watu wa Marekani wanastahili kupata taarifa zaidi kuhusu sakata hilo mara moja.

Mbinu hii imebeba faida kadhaa. Kwanza, Clinton anaweza kuamini kuwa taarifa za kesi hiyo si mbaya kama zinavyojieleza katika vichwa vya habari.

Na kwa sababu hiyo, wapiga kura wataishia kujaza wenyewe wakati maneno kama ‘FBI’ ‘Clinton’ na ‘uchunguzi yanapoonekana katika kichwa cha habari.

Na kwa kusisitiza taarifa zaidi zitolewe, kutamfanya Clinton aonekane machoni mwa umma kuwa hana cha kuficha katika sakata hili.

Hata kama kuna suala baya, kwa namna ambavyo hivi sasa umma unamshambulia Comey kwa kuibua suala hili zikiwa zimebaki siku chache kabla ya uchaguzi, hatokuwa na ujasiri wa kuliendekeza angalau kipindi hiki kabla ya Novemba 8 mwaka huu.

Faida nyingine ni kwamba Clinton anaweza pata huruma ya vyombo vya habari iwapo atakuwa wazi kuruhusu changamoto.

Hata hivyo, umakini wa maneno ya kuzungumza unahitajika ili kuepuka suala hili kuendelea kuwa ajenda kuu katika vyombo vya habari kwa vile mgombea anapokuwa mdomoni mwa vyombo vya habari anakuwa na uwezekano wa kupoteza.

Awali Trump alikuwa wakielekea kupoteza kutokana na kauli zake tata hasa ilipovuja kanda ya video anamosikika akitoa kauli za dhalilishi kwa wanawake, sasa kibao kinaonekana kumgeukia Clinton.

Kuwakusanya Democratic kumshambulia Comey

Wakati Clinton mwenyewe akiwa bado hajashambulia dhamira ya Comey, wasaidizi wake waandamizi kama vile John Podesta tayari wamefanya hivyo. Hata hivyo, kuna hatari ya unafiki hapa kwa vile wasaidizi hao hao walikuwa wakimsifu na kumtetea Comey pale FBI ilipoamua kutomshitaki Clinton Julai mwaka huu kwa sakata la barua pepe.

Lakini pia iwapo Clinton na wasaidizi wake watavishambulia vyombo vya habari kwa namna vilivyoripoti suala hilo, kuna hatari bado kwa vile umma tayari unaamini vyombo vya habari vimejipanga dhidi ya Trump kwa faida ya Clinton.

Hapa Clinton badala ya kuvishutumu moja kwa moja, anaweza kusema kitu kama; vyombo vya habari vimejikita mno katika suala la barua pepe zake kwa gharama ya kila kitu alichowekeza katika uchaguzi huo.

Kuliacha lipite

Kutojitokeza sana na kuliacha sakata hili lipite ili life kifo cha kimya kimya. Lakini hasara ni je itachukua muda gani kwa siku hizi chache zilizobakia?  Katika hili kambi ipataswa ije na mbinu mbadala hapo chini.

Kuibua kashfa nzito dhidi ya Trump

Ili kuzima kila kitu kumhusu kisizungumzwe tena katika dakika hizi za lala salama na hivyo kuwasahaulisha wapiga kura, timu ya Clinton inapaswa itafiti kwa kina iibue bomu zito kummaliza Trump. Kwa kulivujisha kwa vyombo vya habari itakuwa imemaliza kazi bila kujali kama ni mbinu chafu au la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles