NAIROBI, KENYA
KINARA wa Muungano wa Cord, Raila Odinga ameeleza imani yake kuwa atashinda kinyang’anyiro cha urais kwa kura ‘milioni sita’ iwapo wafuasi wake katika maeneo ya Magharibi, Nyanza na Pwani watajiandikisha kwa wingi.
Akihutubia Soko la Koyonzo, Kaunti ya Kakamega, Odinga alisema idadi ya wapiga kura wapya watakaojisajili wakati huu katika kila eneo ndio wataamua mshindi katika kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu.
Aliwasihi wafuasi wake kujiandikisha kwa wingi ili wakizuie Chama cha Jubilee kushinda muhula wa pili.
Odinga alisema upinzani unaazimia kuleta ukombozi wa tatu nchini hapa na una imani kuwa utashinda katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nimeamua kuanza kampeni zangu hapa Matungu kwa sababu ni nyumbani. Mkinipa baraka zenu kwa kujisajili kwa wingi, bila shaka ushindi ni wetu katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti,” alisema.
Odinga alisema upinzani umejipanga sawasawa kwa uchaguzi ujao kwa kuziba mianya yote ya wizi wa kura, akidai hawatalalamika tena kama ilivyokuwa 2013.
“Tuna wafuasi wengi katika maeneo ya Magharibi, Nyanza na Pwani ambao hawajajisajili kuwa wapiga kura. Njia ya kipekee ya kuishinda Jubilee kwa kura milioni sita ni wao kujiandikisha,” alisisitiza Odinga