30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

RAILA ANAJITAFUTIA ADHABU YA KIFO – SERIKALI

NAIROBI, KENYA


MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Kenya, Profesa Githu Muigai, amemuonya Kiongozi wa Muungano wa Upinzani wa National Super Alliane (NASA), Raila Odinga kwamba anakabiliwa na adhabu ya kifo iwapo ataapishwa kuwa ‘rais wa wananchi.’

Katika hilo, Profesa Muigai aliwashutumu mawakili wa upinzani kwa kuwapotosha Wakenya kuhusu kuapishwa kwa Raila, akisema hilo ni kosa la uhaini ambalo hukumu yake ni adhabu ya kifo.

“Inasikitisha kuona baadhi ya mawakili nchini, wenye hadhi ya kuitwa mawakili waandamizi, wanapotosha eti kosa la uhaini halitambuliwi katika Katiba ya sasa,” alisema Profesa Muigai akionekana kumlenga Seneta James Orengo aliyedai kuwa kosa la uhaini halitambuliwi.

Pia anayekabiliwa na hatari hiyo ya kushtakiwa kwa uhaini ni aliyekuwa mgombea mwenza wa Raila wakati wa Uchaguzi Mkuu, Kalonzo Musyoka, ambaye alitarajia kuwasili juzi jioni kutoka Ujerumani, ambako amekuwa akimuuguza mkewe kwa miezi miwili sasa.

Haijafahamika iwapo Musyoka ataapishwa sambamba na Raila, lakini inatarajiwa Makamu Rais huyo wa zamani ataweka wazi mipango yake siku si nyingi kuanzia jana.

Profesa Muigai alisema kitendo hicho ni kinyume cha Katiba na sheria husika, na kuongeza kuwa kuna rais halali ambaye ni Uhuru Kenyatta.

“Idara ya Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Idara ya Mahakama zimejiandaa kupambana na mtu au kundi lolote la watu ambao watathubutu kufanya mapinduzi ya aina yoyote dhidi ya Serikali halali iliyoko mamlakani,” alisema.

Profesa Muigai alisema ni wajibu wa polisi na asasi nyingine huru kuhakikisha kuwa kila Mkenya bila kujali hadhi yake kijamii na kisiasa, anatii sheria.

“Asasi hizi zitatekeleza majukumu yake wakati ufaao, iwapo mtu yeyote atadiriki kuvunja sheria,” aliwaambia wanahabari juzi Jumatatu asubuhi bila kumtaja Raila moja kwa moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles