26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Radi yaua wanafunzi sita darasani

NA EDITHA KARLO, KIGOMA

WATU nane wakiwamo wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Kibirizi mkoani Kigoma, wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi.
Pamoja na vifo hivyo, wanafunzi wengine 15 wa shule hiyo walijeruhiwa vibaya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, Dk. Fadhili Kabaya alithibitisha kupokea miili ya marehemu pamoja na majeruhi.
Alisema tukio hilo, lilitokea jana saa 6 mchana wakati mvua kubwa iliyoambatana na radi ikinyesha.
“Tumepokea majeruhi 15 wa tukio hili, lakini kati yao 10 wametibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuwa nzuri. Wale watano wamelazwa na wanaendelea na matibabu kwa sababu hali zao haziridhishi,” alisema Dk. Kabaya.
Aliwataja waliofariki dunia, kuwa ni Mwalimu Elinaza Mbwambo (25) Forcus Ntahaba (45), mkazi wa Bangwe mjini hapa.
Wanafunzi waliofariki dunia ambao wote ni wa darasa la kwanza shuleni hapo, Dk. Kabaya aliwataja kuwa ni Yusuph Ntahoma (8), Hassan Ally (9), Fatuma Sley (7), Zamda Seif (8), Shukranmi Yohana (7) pamoja na Warupe Kapupa (10).
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa walimu wa shule hiyo, Merina Sililo alisema kabla ya tukio hilo, alianza kuona wingu zito wakati alipokuwa darasani akifundisha.
“Mwanzoni niliona mawingu mazito, kukawa na giza darasani kiasi kwamba nilishindwa kuendelea kuandika ubaoni.
”Baadaye manyunyu yalianza kidogo kidogo, kisha mvua ikaanza kunyesha, ikaanza kuongezeka na kuwa kubwa ikiambatana na radi na ngurumo.
“Ghafla tu, wanafunzi walianguka ovyo darasani na kuzimia, baadaye niliona moto umetanda katika chumba kizima cha darasa, kisha nikaanguka chini na kupoteza fahamu,”alisema mwalimu huyo na kuongeza.
“Nilipozinduka, nilijikuta nikiwa katika Hospital ya Mkoa ya Maweni, nikipatiwa matibabu baada ya kuelezwa nililetwa na walimu wenzangu.
”Kwa kweli, ni Mungu tu ndiye aliyeninusuru kwa sababu tukio lenyewe lilikuwa baya na sijawahi kuliona popote,” alisema mwalimu Sililo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles