27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Wanafunzi Chuo Kikuu Kampala waendelea kugoma

KIUJonas Mushi na Tunu Nassoro, Dar es Salaam
WANAFUNZI wa Kitivo cha Sayansi ya Afya Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) wameendelea kugoma kwa kufunga lango kuu la chuo hicho kuuzuia uongozi kuingia au kutoka hadi malalamiko yao yatakapopatiwa ufumbuzi.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, tangu waanze mgomo Aprili 10 mwaka huu, uongozi wa chuo hicho haujataka kuwasikiliza.
Wakizungumza na MTANZANIA jana, wanafunzi wa chuo hicho waliainisha madai takriban saba wakidai ni ya muda mrefu.
“Tumegoma kwa sababu kwanza kozi zote za sayansi hazijasajiliwa na bodi husika na watu waliohitimu wamenyimwa leseni za kazi,” alisema mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Famasia.
Alisema wanalipa ada kubwa ikilinganishwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza.
“Wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu wanalipa kuanzia Sh milioni 6.5 hadi Sh milioni tisa na kwa mwaka wa kwanza wanalipa Sh milioni tatu,” alisema mwanafunzi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Madai mengine ya wanafunzi hao ni pamoja na kutokuwa na mtaala unaoeleweka, uongozi mbovu akiwamo mshauri wa wanafunzi, programu kuchukua miaka mingi tofauti na vyuo vingine, kushindishwa mitihani kwa makusudi na gharama kubwa ya kurudia mitihani waliyoshindwa.
Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano, Kenneth Uki, alikiri kuwapo madai hayo ingawa mwengine si ya kweli.
Kuhusu kozi kutosajiliwa na bodi husika, alisema ni kweli Bodi ya Famasia haijasajili kozi za famasia huku ingawa alisema si kweli kwamba kozi zote za sayansi hazijasajiliwa.
“Tulishapeleka maombi Bodi ya Famasia tangu 2013 na walikuja kufanya ukaguzi awamu ya kwanza na bado hawajarudi kwa awamu ya pili na ya tatu waweze kutupatia usajili,” alisema Uki.
Akizungumzia ada, Uki alisema tayari yamekwisha kupokewa maombi ya wanafunzi kupunguziwa ada na kwamba kikao cha bodi ya chuo huwa ni mara moja kwa mwaka hivyo wavute subira.
“Ada ni mkataba kati ya chuo na wanafunzi kwa hiyo linapokuja suala la kutaka ipungie ni suala la makubaliano baada ya wanafunzi kupeleka maombi yao… yanaweza yakakubaliwa au kukataliwa, ” alisema Uki.
Hata hivyo alisema wanafunzi wanapochagua chuo hawana budi wasome masharti ya chuo husika ikiwamo ada na kozi zinazotolewa.
Kuhusu madai ya kushindishwa mitihani wanafunzi na gharama kubwa za kurudia mitihani, alisema wanafunzi wamekuwa watoro na kwamba inahitaji fedha kufanya maandalizi ya kurudia mitihani.
Msajili wa Baraza la Wafamasia katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elizabeth Shekalaghe amekiri kuwapo maombi ya usajili kutoka KIU akisema bado zinasubiriwa baadhi ya nyaraka kutoka chuoni hapo.l
“Tulipokea maombi kutoka KIU tukaenda kufanya ukaguzi chuoni hapo na kuwapa masharti na vigezo walivyotakiwa wakamilishe pamoja na kuleta nyaraka, hawakuleta.
“Tukawakumbusha mara mbili Agosti na Septemba mwaka jana bado hawakufanya hivyo ,”alisema Shekalaghe.
Alisema sheria inavitaka vyuo husika visajili kwanza kozi zao na ndipo vifanye udahili wa wanafunzi na kila baada ya miaka mitatu vinatakiwa kukaguliwa upya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles