26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

CWT yafichua siri sekondari kufungwa

Jumanne-SaginiChristina Gauluhanga na Patricia Kimelemeta
CHAMA Cha Walimu Tanzania(CWT) kimefichua siri ya baadhi ya shule za sekondari kufungwa kwa sababu ya kukosa chakula kikisema wakuu wa shule waliochukua uamuzi huo walifuata taratibu zote za sheria lakini serikali haikuwasikiliza.
Chama hicho kimesema kimeshangazwa na kauli ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI,Jumanne Sagini kutangaza kuwachukulia hatua wakuu wa shule hao akisema walikiuka taratibu kabla ya uamuzi wa kuzifunga shule hizo.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema azimio hilo likitekelezwa itakuwa ni kutowatendea haki walimu kwa sababu wao siyo wasambazaji wa chakula bali wanafuata taratibu zilizowekwa.
“Niliwasiliana na walimu wa shule zote zinazodaiwa kufungwa kwa sababu ya njaa lakini walinijibu kuwa kabla ya kufanya uamuzi huo walifuata taratibu za sheria na za kazi ikiwa ni pamoja na kuitisha vikao zaidi ya saba,”alisema Mukoba.
Alisema wakati tatizo linatokea katika shule hizo, walimu hao waliwaita wazabuni na maofisa elimu wa mikoa na wilaya kujadili suala hilo lakini hakukuwapo na utekelezaji wowote, jambo ambalo lilisababisha wanafunzi kuendelea kuteseka na njaa shuleni.
Alisema baada ya kuona hivyo waliamua kuzifunga shule hizo kuwanusuru wanafunzi wasije kupata matatizo zaidi yatokanayo na njaa.
“Serikali inapaswa kulifuatilia suala hili kwa undani kujua kama ni kweli walipeleka fedha hizo, je zilikwenda kwa wakati na kuwafikia walimu hao au ziliishia kwenye mikono ya wakurugenzi?” alihoji Mukoba.
Alisema ni vema serikali iwe makini na kuhakikisha fedha zinapelekwa kwa wakati na kuwafikia walengwa ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema CWT inafuatilia kwa undani hatua hiyo ya serikali na kama itatekeleza tishio lake kwa walimu hao wakuu basi kitaamua nini cha kufanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles