Na ELIUD NGONDO, SONGWE
SIKU mbili baada ya radi kuua ng’ombe 10 na kuharibu mazao katika Kijiji cha Lali Kata ya Ibaba Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, tukio hilo limejirudia tena ambapo safari hii imeua mifugo 14.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Lali, Julius Mwazembe, alisema kuwa tukio la awali lilitokea mwishoni mwa wiki na la pili lilitokea juzi ambapo mzee mmoja ajulikanaye kwa jina la Koned Mwazembe (58) ambaye ndiye mmiliki wa mifugo hiyo pamoja na mjukuu wake Zawadi Ally (13) walinusurika.
Alisema kuwa mzee Mwazembe akiwa anachunga mifugo hiyo ilianza kunyesha mvua kubwa hivyo yeye pamoja na mjukuu wake waliamua kusimama chini ya mti huku mifugo ikiwa imejificha kwenye kichaka umbali wa mita 30 kutoka walipokuwa.
Mwazembe alisema kuwa wakati mvua hiyo ikiendelea kunyesha, radi ilipiga bila wao kujua ilipotua, lakini baadaye baada ya kuacha waliamua kwenda kusaka mifugo hiyo na kukuta ng’ombe wawili, mbuzi tisa na kondoo watatu wamepigwa na radi na kufa.
“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa alimnusuru mzee pamoja na mjukuu wake ambao walikuwa umbali wa kama mita 30 kutoka eneo lilipotokea tukio hilo, hatuelewi tatizo ni nini maana hili ni tukio la pili ndani ya siku mbili na kwa wananchi waliopoteza mifugo yao wamepata hasara kubwa,” alisema Mwazembe.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Tata kibona, alisema kuwa matukio hayo yameonekana kuwa sio ya kawaida na kwamba kwa sasa wananchi wengi wameanza kupatwa na wasiwasi kwamba pengine wanaweza wakaendelea kupata madhara.
Alisema kuwa wao kama viongozi wa Serikali wamekubaliana kuitisha mkutano wa dharura kwa ajili ya kujadili hali hiyo na kuona namna ya kuweza kujiweka salama kutokana na madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha.
Alisema kuwa hasara ambayo imetokea kutokana na mvua hiyo ni kubwa kwa maelezo kuwa ndani ya siku tatu mifugo 24 kufa sio jambo la kawaida kutokea.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude, alikiri kutokea kwa matukio hayo na kwamba chanzo ni kijiji hicho kuwa katika eneo la mwinuko ambao ndipo mvua inapoanzia kunyesha.