MOSCOW, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, amesema kwamba, Serikali yake inaunga mkono kwa dhati wazo la kuanzisha soko huru katika nchini za Bara la Asia na Pasifiki.
Rais Putin alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kupitia taarifa yake iliyotolewa na Wizara ya Habari nchini hapa na kusambazwa katika vyombo mbalimbali vya habari.
Katika taarifa hiyo, Rais Putin, alisema kwamba kwa kuanzishwa soko hilo kutachochea maendeleo ya haraka kibiashara baina ya nchi hizo zilizopo katika ukanda huo wa Asia na Pasifiki.
“Tunaunga mkono kwa dhati wazo la kuanzishwa soko huru kwa nchi za bara la Asia na Pasifiki,” ilieleza taarifa hiyo iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari nchini hapa.
“Tunaamini kwamba, hatua hii ni kwa ajili ya manufaa yetu na inaonyesha fursa ya kuimarisha nafasi zetu katika masoko ya APR ambayo yanakuwa kwa kasi. Nataka kutambua kwamba zaidi ya miaka mitano iliyopita, sehemu ya uchumi wa APEC katika biashara ya nje ya Urusi imeongezeka kutoka asilimia 23 hadi 31 na kutoka asilimia 17 hadi 24 katika mauzo ya nje. Na hatuna nia ya kuishia hapo,” iliongeza taarifa hiyo.
Akiunga mkono zaidi hatua hiyo, Rais Putin, alisema mradi huu utakaoanzishwa unapaswa kutekelezwa kwa sababu ya uzoefu wa muundo muhimu wa ushirikiano katika nchi za Asia, Pasifiki na Eurasia, hasa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasian (EEU) ambapo Urusi inashirikiana na Armenia, Belarus, Kazakhstan na Kyrgyzstan.
Alisema umoja wao umeendelea kuimarika kwa nguvu na akasema kuwa wanatamani kujenga uhusiano na nchi zote na vyama ambavyo vina nia ya kufanya hivyo.