25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP, PUTIN KUPAMBANA NA ISIS

DA NANG, VIETNAM

RAIS wa Marekani, Donald Trump na Vladimir Putin wa Urusi, wamekubaliana kuhakikisha wanapambana kwa nguvu zote ili kundi la wapiganaji wanaojiita Islamic State (IS) linashindwa vita nchini Syria.

Kwa mujibu wa maofisa wa rais wa Urusi, wamesema viongozi hao wawili wamekutana jana kwa muda mfupi pembezoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi za Asia na Pasific nchini Vietnam.

Viongozi hao wawili walikutana mara tatu katika kipindi cha saa 24 katika mji wa Da Nang. Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa Serikali ya Marekani kuhusu tamko lililotolewa na Serikali ya Urusi.

Mkutano kati ya Rais Trump na Vladimir Putin, ulitarajiwa kufanyika wakati wa mkutano huo wa APEC, lakini ni maelezo machache sana ambayo yametolewa.

Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza Julai katika mkutano wa nchi tajiri zaidi duniani, G20 katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani.

Maswali kuhusu uhusiano wa Donald Trump na Urusi yamekuwa yakiulizwa mara kwa mara. Wasaidizi wake wakuu wa zamani wanachunguzwa kwa tuhuma za kushirikiana na Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2016. Lakini Serikali ya Urusi imekanusha tuhuma hizo.

Ingawa Ikulu ya Marekani haijasema chochote kuhusu mkutano wa wawili hao, taarifa ya Kremlin iliyotolewa jana imesema viongozi hao waliafikiana kwamba mzozo wa Syria hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi.

Aidha, viongozi hao wamekaririwa wakisema kujitolea kwao kutasaidia kuwashinda magaidi wa ISIS na kuzitaka pande zote kushiriki mazungumzo ya amani ya Geneva.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Interfax la Urusi, wameahidi kuendelea kudumisha njia za mawasiliano za kijeshi kati ya majeshi ya Urusi na Marekani kuzuia uwezekano wa kushambuliana na IS.

Urusi imekuwa ikiunga mkono Serikali ya Rais Bashar al-Assad katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu miaka sita sasa. Marekani nayo huwasaidia waasi wa makundi ya Waarabu wa Syria na Wakurdi.

Tangu 2014, Marekani imeongoza muungano ambao umekuwa ukitekeleza mashambulio ya kutoka angani dhidi ya ISIS nchini Syria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles