Na Ramadhan Hassan, Dodoma
MATATIZO katika ndoa, ugumu wa maisha,u kosefu wa chakula,vimetajwa ni visababishi vya magonjwa ya akili wakati wa kipindi cha uzazi.
Hayo yameelezwa na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Agha Khan cha Jijini Dar es salaam, Profesa Tumbwene Mwansisya wakati akizungumza katika mafunzo kwa wahudumu 29 wa sekta ya afya Jijini Dodoma juu ya kumtambua mtu mwenye ugonjwa wa akili na jinsi ya kumtibu katika kipindi cha uzazi.
Profesa Mwansisya amesema sababu ya ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa akili katika kipindi cha uzazi ni mahusiano ambapo amedai ndoa nyingi zimekuwa na changamoto hali ambayo inafikia mama mjamzito kuwa na mawazo mengi hivyo kupata ugonjwa huo.
“Siku hizi kunachangamoto sana katika mahusiano watu wenye ndoa ndio wanauana sana,ugumu wa maisha,kukosa chakula hivyo kukosa matunzo na pia jamii inavyomchukulia mtu.Matatizo yanaweza yakawa kwa mtu ama mabadiliko ya homoni au changamoto za maisha,”amesema Prof.Mwansisya.
Prof.Mwansisya amesema madhara yake ni kwa mama hawezi kuwa na mahusiano mazuri na mme wake na mtoto wake wa kumzaa ambapo pia amedai kutakuwa na shida katika jamii kwani baba anaweza kuanzisha familia nyingine.
Amesema tiba yake ni dawa ,matibabu ya kisaikolojia kwa kupewa ushauri nasaha,matibabu ya kijamii na matibabu ya kiroho.
Akielezea mafunzo hayo amesema yamelenga jinsi gani ya kutambua mtu mwenye ugonjwa wa akili jinsi ya kumtibu na kuzuia mama ama baba anaenda Kliniki kwa ajili ya uzazi na jinsi gani aweze kutibiwa.
“Kwa kawaida kipindi cha uzazi huwa kinaambatana na magonjwa ya akili lakini kwa bahati mbaya sana kipindi hichi cha uzazi wengi hawajafundishwa jinsi ya kutambua magonjwa ya akili na jinsi ya kutibu ndio maana tukaja na mafunzo haya ili kuweza kuitatua hii changamoto,”amesema Profesa Mwansisya ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya akili,”amesema
Amesema wamekuwa wakifundisha magonjwa gani ya akili ambayo yamekuwa yakitokea,jinsi ya kutambua kama mama mjamzito ana ugonjwa huo pamoja na jinsi ya kumtibu.
Prof. Mwansisya amedai kwa pomoja wamejadiliana mikakati ya kuangalia jinsi ya kutengeneza huduma kwenye kadi ya mama ili mama mjamzito aweze kuulizwa maswali pindi anapofika Kliniki ili iwe rahisi kuweza kujua tatizo mapema.
Amesema tatizo hilo ni kubwa kwani utafiti mwingi umekuwa ukifanywa mjini bila kufika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake,Daktari wa Afya ya akili kutokea kituo cha afya cha Makole,Zahati Shamahonge amesema mafunzo hayo yamemsaidia kupambanua, kujua mama anapokuwa mjamzito kuna mabadiliko ambayo yanatokea mwilini mwake hivyo anatakiwa kupewa huduma zipi ili kuweza kujua tatizo.
“Inapelekea yule mama kubadilika kitabia kimaono na vitendo mama mjamzito anapopata mimba jamii inatakiwa imsapoti kuanzia lishe na kila kitu,kuna wengine wanapata mimba za utotoni tusimshangae tukimshangaa anaanza kuhisi vibaya na anaanza kupata msongo wa mawazo,”amesema
Naye,Mratibu wa afya ya akili Wilaya ya Dodoma Mjini,Asnati Mgeni amesema mafunzo hayo yamemsaidia kujua jinsi gani ya kuwasaidia wenye matatizo pamoja na kujua ukubwa tatizo.
“Saa zingine watu walikuwa wanajua kwamba kalogwa au hachangamani kumbe ni shida ambayo anakuwa ameipata katika akili zake,”amesema.
Amesema katika Wilaya ya Dodoma tatizo hilo ni kubwa kwani asilimia zaidi ya 80 wana tatizo hilo huku wengi wakiwa hawajui.