Na MWANDISHI WETU, Kondoa
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amewataka wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya wasichana Kondoa, kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kuachana na mambo ambayo hayana tija kwa maisha yao.
Aliyasema hayo jana mjini hapa wakati wa mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo.
Alisema mitihani si muujiiza kwa mwanafunzi hivyo hawana budi kusoma kwa bidii waweze kufikia malengo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Waziri aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanatumia uhuru wa vyuoni vizuri watakapochaguliwa kujiunga na vyuo kwa vile maisha ya elimu ya juu hayana ulinzi kama wa shule.
“Napenda kuwasihi sana wanangu kuwa mnapokaribia kumaliza elimu yenu hii ya sekondari na kwenda kujumuika na jamii nendeni mkaendeleze nidhamu na matendo mema ambayo walimu wenu wamewafundisha hapa shuleni.
“Msiende kujiingiza kwenye majanga ya Ukimwi, dawa za kulevya na sitegemei muende mkapotoke,” alisema Profesa Ndalichako.
Mkuu wa shule hiyo, Flora Nusu, alisema changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi yakiwamo Fizikia, Kemia, Biolojia, Hisabati .