27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

PROF.MRUMA WA KAMATI YA MAKINIKIA ATEULIWA TENA

Na AGATHA CHARLES

-DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa kamati ya kwanza ya wanasayansi iliyoundwa kuchunguza mchanga wa madini uliokuwa kwenye makontena 277 yaliyozuiwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi, Profesa Abdulkarim Mruma, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER).

Uteuzi huo, uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli, ulitangazwa jana kupitia taarifa iliyosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Profesa Mruma, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia nchini, ameteuliwa wakati ambao mazungumzo ya wataalamu wa Serikali na wale wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation yakiendelea kuhusu makinikia, ambayo yamezuiwa kusafirishwa nje ya nchi.

Itakumbukwa Mei 24, mwaka huu, Profesa Mruma kupitia Kamati yake iliyoteuliwa na Rais Magufuli, iliyokuwa na wajumbe nane, ilibaini makontena hayo 277 yaliyozuiwa Bandari ya Dar es Salaam yana tani 7.8 za dhahabu, yenye thamani ya kati ya Sh bilioni 676 na Sh trilioni 1.147.

 

Kiwango hicho kilitajwa kuwa ni kikubwa, kikilinganishwa na kile ambacho Kampuni ya Barrick ilidai kukikuta.

Licha ya hilo, Profesa Mruma, ambaye ndiye alisoma mapendekezo tisa ya kamati, katika ripoti hiyo moja ilikuwa ni lile la kuendelea kusitisha usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi hadi mrabaha stahiki utakapolipwa.

Mjadala wa makinikia wa ripoti hiyo na ile ya pili iliyochunguza athari za kisheria na kiuchumi kuhusu usafirishwaji wa mchanga, zote zilijadiliwa katika Bunge lililopita, ambalo kwa asilimia kubwa liliunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Juni mwaka huu, Kampuni ya Acacia, ambayo Barrick ni mmiliki wake mkubwa, ilizikataa taarifa zote zilizotolewa kwenye ripoti hizo kwa madai kuwa inafanya shughuli zake kwa kiwango cha juu na kufuata sheria.

Juni 14, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick, Profesa John Thornton, alilazimika kuja nchini na kukutana na Rais Dk. Magufuli Ikulu kujadili suala hilo.

Profesa Thornton alisafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada na kutua nchini, akiiwakilisha Barrick, ambayo inaendesha shughuli za uchimbaji wa madini nchini.

Kukutana huko kulizaa mazungumzo yanayoendelea hadi sasa baina ya Barrick na Serikali, ambayo bado haijulikani yatakwisha lini na mwafaka wake ukoje.

Sambamba na Mruma, Rais Magufuli pia amewateua maprofesa wengine wawili kuongoza taasisi ya mafuta na moja ya elimu.

Maprofesa hao ni Joseph Buchweshaija, ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania Ltd, pia ni Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Mwingine ni Prof. Evaristo Liwa, ambaye anakuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (Ardhi University), akichukua nafasi ya Prof. Idrissa Mshoro, ambaye amestaafu.

 

 

Taarifa nyingine iliyotolewa baadaye jana jioni na Ikulu ilieleza kuwa, Rais Magufuli alimteua Jaji Barke Mbaraka Sahel kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal-FCT), akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Zainab Muruke, aliyemaliza muda wake.

Jaji Sahel kabla ya uteuzi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, ambayo wajumbe wake ni Mustafa Siyani, Donald Chidowu, Susan Mkapa,  Bitamo Phillip, Yose Mlyambina na Theodora Mwenegoha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles