Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji,Prof.Kitila Mkumbo amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano nchi imeendelea kujitosheleza kwa chakula huku kukuendelea kuwa na utulivu,amani na mshikamano.
Kauli hiyo ameitoa Aprili 17,2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano ambapo Prof Kitila amesema Nchi inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124.
“Sisi katika miaka 60 tumetoka mbali kwa sasa katika chakula tunajitosheleza kwa asilimia 124 na tunataka mwakani tufikishe asilimia 130.Uhai wa nchi hii upo salama,”amesema Prof Kitila.
Aidha,Prof Kitila amesema katika kipindi cha miaka 60 Nchi imeendelea kuwa na amani,utulivu na mshikamano huku akiwapongeza wananchi na Serikali kwa kuhakikisha jambo hilo linaendelea kudumu.
“Tunafahamu kuna baadhi ya nchi wanatafuta amani sisi tumefanikiwa kuilinda amani,utulivu na mshikamano ndio maana tarehe 26 tutaadhimisha miaka 60,”amesema Prof Kitila.
Katika sekta ya elimu,Waziri Kitila amesema cchi imepiga hatua kubwa kwani zaidi ya asilimia 69 ya wanafunzi wapo shuleni huku malengo yakiwa ifikapo 2025 iwe asilimia 100.
“Kuna mambo unatakiwa kufanya kama binadamu ili uweze kuongeza ustawi cha kwanza ni kumpa elimu ili aelimike na katika kipindi cha miaka 60 Serikali imeendelea kuweka mkazo kuhakikisha wananchi wake wanapata elimu,”amesema Prof Kitila.