TAKWIMU zinaonesha kuwa usafiri wa anga ni wa pili kwa usalama duniani baada ya treni. Takwimu hizi hulinganisha idadi za ajali ambazo hutokea katika kila sekta ya usafiri. Dhana hii ya usafiri wa anga kuwa usafiri salama zaidi haiishii tu hapo kwenye ulinganifu wa ajali bali pia wataalamu wanaeleza kuwa, kwa kiwango cha asilimia 99 abiria ana nafasi ya kupata ajali akiwa njiani kuelekea Airport kuliko akiwa kwenye ndege.
Viwango hivi vya usalama katika sekta ya anga havijafikiwa kwa bahati, ila ni kutokana na ukweli kwamba usafiri wa anga una usimamizi madhubuti na hiyo ndiyo sababu kubwa ya mafanikio ya usalama katika sekta hii. Ajali chache ambazo hutokea hufanyiwa uchunguzi wa kina na matokeo ya uchunguzi huo hutumika katika kuboresha upungufu uliobainika ili kuepusha ajali hizo kujirudia.
Hapa nchini kama ilivyo duniani kote, matukio ya ajali za ndege ni machache. Hii inatokana na usimamizi madhubuti wa Mamlaka ya Anga (TCAA) katika kusimamia sekta hii. Pamoja na kuwa na mashirika ya ndege yanayotoa huduma zenye viwango.
Precision Air ni moja ya mashirika ya ndege ya kizawa ambayo yametutoa kimasomaso katika viwango vya kimataifa. Kwa sasa shirika la Precision Air ndilo pekee nchini Tanzania linalotambuliwa na taasisi ya kimataifa ya ukaguzi wa usalama na viwango kwa mashirika ya ndege duniani IOSA, iliyoko chini ya umoja wa mashirika ya ndege duniani IATA.
Precision Air hujifanyia matengenezo ya ndege zake yenyewe. Hii ni kwa sababu ni shirika pekee lililopata cheti cha AMO (Aircraft Maintanance Organisation) yaani cheti kinachoitambua Precision Air kama shirika linaloweza kutoa huduma ya ukarabati wa ndege. Cheti hiki hutolewa baada ya TCAA kukagua uwezo wa kitaaluma na miundombinu ya shirika na kujiridhisha kuwa shirika husika lina uwezo wa kutoa huduma ya matengenezo ya ndege.
Cha kufurahisha zaidi ni kwamba Precision Air imejijengea uwezo katika kitengo cha ufundi hata kuweza kutoa huduma kwa mashirika mengine ya ndege.
Kitengo cha ufundi na matengenezo cha Precision Air kinaundwa na wafanyakazi wapatao 79, ambao kati yao Mainjinia ni 13, 34 ni mafundi na waliobakia wako katika vitengo vya maktaba, mipango, usimamizi wa viwango na watunza kumbukumbu. Timu hii ya ufundi inajumuisha wataalamu waliobobea katika nyanja tofauti.
Kitengo hiki cha ufundi kinaongozwa na Injinia Genaro Sicurreza, ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka 48 katika sekta ya anga. Injinia Genaro anaeleza kuwa kwa zaidi ya miaka 10 aliyofanya kazi Precision Air amekuwa na lengo moja tu la kuhakikisha anatengeneza timu ya Watanzania yenye uwezo wa hali ya juu katika nyanja ya ufundi wa ndege, jambo ambalo anaamini amefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90.
Anaongeza zaidi kuwa Precision Air imefanya jitihada mbalimbali katika kujenga uwezo wa mafundi wake, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka nje kwa masomo maalumu ili kuhakikisha mafundi hawa wanajengewa uwezo wa hali ya juu katika utendaji wao. Anajivunia pia timu yake kuwa na leseni ya EASA PART 66 ambayo ni kiwango cha juu cha usalama kinachotambulika duniani.
Hivi karibuni, takribani mafundi tisa walishiriki katika mtihani wa kupata leseni ya EASA na wanane walipasi mitihani yao. Kushiriki katika mafunzo haya na kufaulu kunawafanya kuingia katika kundi la mafundi wenye viwango vya juu kabisa nchini.
Injinia Stansilaus Maganga ambaye ni Mkaguzi wa Viwango katika kitengo cha ufundi Precision Air ni mmoja kati ya matunda ya programu mbalimbali za kuendeleza uwezo wa mafundi wa ndege zinazofanywa na Preecision Air ambapo amekuwa Mtanzania wa kwanza kupata leseni ya EASA PART 66. Leseni ambayo inatambulika duniani kote.
Shabani Hashim ambaye ni Meneja Huduma za Ufundi Precision Air, anasema anajisikia fahari kuongoza timu ya ufundi ya Precision Air yenye uwezo mkubwa katika utendaji wake. Injinia Hashim anadokeza kuwa lengo lao kubwa katika majukumu yao ya kila siku ni kuhakikisha Precision Air inafanya safari zake na ndege zilizo imara na salama.
“Ili abiria waweze kusafiri wanahitaji ndege iliyo salama. Kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ndege za Precision Air hufanyiwa ukaguzi kila siku kabla na baada ya safari, ili kubaini kama kuna changamoto za kiufundi ili zifanyiwe kazi. Haya yote tunayafanya tukiwa na jambo moja kichwani ambalo ni Usalama wa abiria, kuna wakati tunalazimika kuchelewesha safari ili tu kuhakikisha ndege iko katika hali nzuri na haitohatarisha maisha ya abiria. Mara nyingi tunawaudhi abiria ila jambo ambalo tunatamani waelewe ni kuwa tunajali usalama wao kuliko kitu kingine chochote,” anaeleza Injinia Shabani.
Kama ilivyo nadra kusikia matukio ya ajali za ndege katika anga za Tanzania, timu ya ufundi ya Precision Air nayo inajivunia kuchangia katika mafanikio hayo kwa kuhakikisha ni kati ya mashirika yenye safari nyingi nchini Tanzania inafanya safari zake salama.
Katika muendelezo huu wa kuangalia kitengo cha ufundi cha Precision Air, tutazame Hangar (Eneo maalumu la maegesho na matengenezo ya ndege) la shirika hili. Precision Air ndilo shirika pekee nchini Tanzania lenye Hangar ya kisasa kabisa inaloweza kuhudumia ndege tano aina ya ATR kwa wakati mmoja au ndege kubwa aina ya Boeig au Air Bus mbili kwa wakati mmoja.
Precision Air inafanya safari kuelekea zaidi ya maeneo 12 ikitokea Dar es Salaam ambapo ndio makao makuu ya Shirika hilo. Maeneo inapofika Precision Air ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Zanzibar, Mwanza, Musoma,Bukoba, Tabora, Pemba, Mtwara, Nairobi na Comoro.
Hili linadhihirisha ukubwa wa jukumu walilonalo kitengo hiki cha ufundi Precision Air kwani ili shirika liweze kuendesha safari hizi kwa ufanisi basi ndege zinabidi ziwe katika hali nzuri kwa safari.