23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 2, 2024

Contact us: [email protected]

PPRA yawafunda watumishi wa umma matumizi ya mfumo wa manunuzi kielektroniki

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAKATI Sheria Namba 10 ya mwaka 2023 ya ununuzi wa Umma ikianza kutumika Juni 17, mwaka huu na kanuni zake zikisubiriwa kuanza Julai Mosi, mwaka huu, Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendelea kuwanoa wataalam wa idara za ununuzi katika taasisi tumizi kuhusu Mfumo wa manunuzi ya Umma Kielektroniki (NeST) ili kuwa tayari kuutumia na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Katika kutekeleza hilo PPRA imeanza mafunzo mahususi ya ya kuwaongezea ujuzi watumiaji wa mfumo huo hususani wakuu wa taasisi, wajumbe wa bodi za zabuni, vitengo vya usimamizi wa ununuzi (PMU), idara tumizi, wakaguzi wa ndani, maafisa sheria, na wataalam wa mifumo wa taasisi zaidi ya 60 kuhusu kuchakata ununuzi kupitia mfumo wa NeST, ambayo yameanza leo Juni 24 hadi 28, mwaka huu jijini Mwanza.

Akizungumzia mafunzo hayo, Meneja wa Huduma za Kanda Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Juma Mkobya, amesema lengo ni kuendelea kuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo katika taasisi nunuzi kwa kuzingatia kuwa mfumo huo umeongezewa moduli na maboresho, hivyo ni muhimu watumiaji wake wakaendelea kupatiwa mafunzo ili kuwawezesha kutekeleza shughuli za ununuzi wa umma kwa ufanisi na kupata thamani ya fedha.

Amesema mafunzo hayo ni kwa ajili ya kujengeana uwezo namna ya kufanya manunuzi kutumia mfumo wa NeST ambao umeweka uwazi, uwajibikaji na umepunguza mianya ya rushwa kwa sababu wazabuni na maafisa ununuzi hawaonani, huku akiishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kujenga mfumo huo ambao unasaidia katika kazi za ununuzi.

“Matarajio yetu ni kwamba baada ya mafunzo haya watumishi wa umma wataweza kufanya shughuli za ununuzi kwenye mfumo kuanzia wanapoanzisha mahitaji mpaka wanapotangaza zabuni na kutoa tuzo za mikataba kwa ufanisi,” amesema Mhandisi Mkobya na kuongeza;

“Wito wangu ni kwamba wajitahidi kuhakikisha kwamba manunuzi yote yanatumia mfumo wa NeST kwa sababu kwa sasa ni takwa la kisheria hauwezi kufanya manunuzi yoyote nje ya mfumo. Vilevile, waendelee kujifunza na mamlaka itaweka mpango maalum wa kutoa mafunzo kwa ajili ya mfumo, sheria na kanuni zake,” amesema.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Alfred Manda amesema kupitia mfumo huo washiriki hao wakielimishwa watatatua changamoto mbalimbali zikiwemo uwasilishaji wa nyaraka kwa wakati, kusaini nyaraka na uanzishaji wa mahitaji kwa haraka kwani mfumo huo hutumia muda mfupi na taarifa zote zitapatikana, hivyo, kutatua changamoto ya manunuzi yaliyokuwa yanaibuka bila kufuata taratibu.

“Kwahiyo kutakuwa na uwajibikaji na uwazi wa hali ya juu kwenye mfumo kwasababu kila mmoja anatakiwa afanye kazi zake kama mfumo wa ununuzi unavyoelekeza kwenye sheria yetu, ambalo hili lilikuwa halizingatiwi kwa kiwango kikubwa nje ya mfumo,” amesema Manda na kuongeza;

“Washiriki watajifunza kuhusu usajili kwenye mfumo, kuandaa mahitaji ya mwaka mzima, kuandaa mpango wa ununuzi, namna ya kuanzisha michakato ya tenda, kuandaa mahitaji ya ununuzi wa jenzi mbalimbali, uandaaji wa nyaraka za zabuni, kufanya ufunguzi wa zabuni kwenye mfumo, na kuandika muhtasari wa vikao, kufanya tathmini na namna ya kusimamia mikataba kielektroniki,” ameeleza

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Happiness Komba kutoka halmashauri ya wilaya ya Itilima, Singida, amesema matarajio yake ni kujifunza na kuelewa ili awe mbobezi katika mfumo huo na kuhakikisha halmashauri ya Itilima wanaelewa vizuri na kuufanyia kazi vyema ili kila kitu kipitishwe ndani ya mfumo kama sheria inavyoelekeza.

Displaying B.JPG

“Nimekuja kujifunza zaidi kuhusu huu mfumo wa NeST na sheria mpya ambayo inaanza kutumika kipindi hiki, ni mfumo mzuri kuna uwazi wa kutosha na ukiangaza tenda wazabuni wengi wanaomba na unapata mzabuni stahiki kulingana na vigezo na mfumo hauna usumbufu,” amesema Happines.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles