NA MWANDISHI WETU
TAMASHA la Pop Up Bongo limevutia mamia ya watu ambao walifika kushuhudia, kununua bidhaa za wajasiriamali wa kazi za ubunifu pamoja na kupata burudani ya muziki.
Tamasha hilo la saba lilifanyika kwenye mgahawa wa Tuk Tuk Thai uliopo Masaki ambapo ulihusisha wajasiriamali mbalimbali wa kazi za ubunifu.
Mratibu wa tamasha hilo, Natasha Stambuli, alisema kuwa tamasha la mwaka huu limeshuhudia wabunifu wengi wa ndani, huku hamasa kubwa ikiongezeka kwa watu kuhudhuria na kununua bidhaa za ubunifu.
“Lengo la tamasha hili ni kuwakutanisha wajasiriamali wa bidhaa za ubunifu na wanunuzi kwa maana ya wateja ili wawaunge mkono na tunaishukuru kampuni ya Bia ya Serengeti ambao wametudhamini kupitia kinywaji chao cha Smirnoff,” alisema.
Kwa upande wake Meneja wa vinywaji vikali wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Shomari Shija, alisema kampuni hiyo imeamua kudhamini tamasha hilo kwa kuwa inatambua mchango wa ujasiriamali nchini.