24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi watatu na Mfanyabiashara kizimbani kwa uhujumu uchumi

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Askari watatu na raia watano akiwemo Mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite jijini Arusha, Lucas Mdeme (46) mkazi wa Njiro jana walipandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Arusha wakikabiliwa na mashtaka sita ikiwemo uhujumu uchumi, utakatishaji fedha haramu na kupanga njama za kujipatia fedha ya awali Sh milioni 10 kati ya Sh milioni 30 walizohitaji kutoka kwa, Sammy Mollel. 

Askari watatu waliofukuzwa kazi kwa tuhuma ya rushwa na kupandishwa kizimbani jana ni pamoja na pamoja na Askari mwenye namba G. 5134 DC Heavenlight Mushi aliyekuwa Askari kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni jijini Dar es Salaam, H.125 PC Gasper Paul kitengo Cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma na H.1021 PC Bryton Murumbe aliyekuwa Askari wa kawaida mkoani Dodoma.

Raia waliopandishwa mahakamani mbali ya Mdeme wengine ni pamoja na Joseph Chacha(43) maarufu kwa jina la ‘baba Ngodo’ mkazi wa Ilboru, Leonila Joseph(46) mkazi wa Ilboru, Mfanyabishara maarufu jijini Arusha, Nelson Lyimo(58) mkazi wa Kijenge Juu na Omary Alphonce (43) maarufu kwa jina la Matelephone mkazi wa Olasiva jijini Arusha.

Wakisomewa mashtaka na Waendesha Mashtaka Waandamizi wa Serikali, Adelaide Kassalay na Agnes Hyera mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Arusha, Rose Ngoka walidai kuwa shitaka la kwanza linawakabili mshitakiwa wa 1, 2, 3 ambao ni Askari kuwa Desemba 5, mwaka jana walijihushisha na uhalifu huku wakitambua kuwa wao ni watumishi wa umma na kujipatia rushwa ya awali ya kiasi cha Sh milioni 10 kutoka kwa, Sammy Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha.

Kassalay alisoma shitaka la pili linalowakabili washitakiwa wanne ambaye ni Baba Ngodo, mshtakiwa wa tano Joseph, mshtakiwa wa sita Lyimo, mshtakiwa wa saba Mdeme na mshtakiwa wa nane Matelephone wote wanashtakiwa kwa kujifanya watumishi wa umma na kuunda mtandao wa kihalifu na kupanga njama za kujipatia fedha taslimu Sh milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Mwendesha mashitaka huyo alisoma shtaka la tatu linalowakabili watuhumiwa wote nane ambalo ni la kupanga njama za kuhujumu uchumi kwani Desemba 5, mwaka jana waliweza kujipatia fedha Shy milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Alisema shitaka la nne linamkabili Chacha mshitakiwa wanne ambaye anatuhumiwa akiwa na nia kufanya uhalifu na udanganyifu na kujitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa Umma Ikulu.

Mwendesha mashitaka huyo alisoma shtaka la tano linalowahusisha washitakiwa wote kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kiasi cha Sh milioni 10 za awali kati ya Sh milioni 30 ili wamwachie huru kwa tuhuma za kukwepa kodi na kufanya biashara ya madini ya Tanzanite kwa kutorosha madini nje kinyume cha sheria.

Kassalya alisoma shitaka la sita la utakatishaji fedha haramu linalowakabili washitakiwa wote kwani ilidaiwa mahakamani hapo kuwa wote kwa pamoja Desemba 5, mwaka jana walipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara Sammy Mollel.

Mara baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Ngoka aliwaeleza watuhumiwa wote kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashitaka hayo na watuhumiwa wataenda rumande hadi Januari 27, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles