VERONICA ROMWALD NA GODFREY MBANILE (GPC), DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi limesema limeimarisha ulinzi kesho wakati wa kuapishwa Rais mteule wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli.
Sherehe za kuapishwa Dk. Mgufuli zitafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Oparesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alisema ni marufuku kwa wananchi kushiriki katika maandamano yaliyoandaliwa bila kufuata taratibu za nchi.
“Tunawashukuru wananchi na vyombo vya habari kwa sababu kwa pamoja tulishirikiana katika kipindi cha uchaguzi ambacho kilikuwa ni cha vuta nikuvute na tumeweza kuilinda amani yetu hadi hii leo.
“Hatimaye kesho tunatarajia kuapishwa kwa rais mteule, Dk. Magufuli, nawasihi wote kwa pamoja tuendelee na moyo huo huo wa kulinda amani yetu.
“Tusishiriki kabisa maandamano batili kwa sababu yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani na jeshi hatutasita kuwachukulia hatua watu watakaokaidi agizo hili,” alisema.
Aliwataka wananchi na waandishi wa habari kutoa ushirikiano wakati wa kuapishwa kwa Dk. Magufuli kwa kutoa taarifa iwapo watabaini kuwapo viashiria vya uvunjifu wa amani kama walivyofanya katika kipindi cha kampeni na uchaguzi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa,” alisema.
Akizungumzia maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyotarajiwa kufanyika jana, alisema polisi walilazimika kuyazuia kwa vile yalikosa sifa kutokana na maombi kuwasilishwa nje ya muda unaotakiwa.