30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

POLE DK. MPANGO, LAKINI USIMLAUMU BOSI WAKO

MWANZONI mwa wiki hii Bunge limepitisha Bajeti ya zaidi ya Sh. trilioni 31. Kama ilivyo ada, Bajeti hiyo kwa ajili ya mwaka wa fedha 2017/2018 imepitishwa baada ya mjadala uliodumu kwa muda wa siku saba.

Alipowasilisha Bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alishangiliwa sana na wabunge wengi, hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kushangilia kwao kulitokana na wao kuamini kuwa Bajeti iliyowasilishwa ilikuwa mzuri sana.

Hiyo ilikuwa ni dalili moja kuwa Dk. Mpango asingepata shida sana kuitetea Bajeti yake mbele ya wabunge.
Lakini mara baada ya Dk. Mpango kuwasilisha Bajeti hiyo, akapata mteremko mwingine.

Rais Magufuli akapokea ripoti ya pili ya kamati aliyoiunda kuchunguza suala la makinikia. Ripoti ilikuwa imejaa mambo mengi lakini kubwa ilikuwa inaonyesha kuwa kwa zaidi ya miaka 20 Kampuni ya Acacia, inayomiliki migodi mitatu ya dhahabu hapa nchini, imekuwa ikiibia nchi.

Ripoti hiyo ilikuwa ni mteremko mwingine kwa Dk. Mpango bungeni kwa sababu badala ya kujadili Bajeti, wabunge wengi waliutumia muda mwingi wa mjadala huo kujadili suala hilo la Acacia na makinikia.

Huu unaweza kuonekana kama mteremko kwa Dk . Mpango kwa sababu mawaziri wengi hupata shida sana kuzitetea Bajeti zao bungeni. Wabunge wanawabana kwa mambo kadhaa na wakati mwingine wanatishia kukwamisha Bajeti hizo. Hali haikuwa hivyo kwa Dk. Mpango kwa sababu wabunge wengi walishaonyesha kufurahishwa na Bajeti yake na pia ripoti ya makinikia.

Lakini mteremko huu alioupata Dk. Mpango ni wa kumuumiza. Mawaziri ambao wanabanwa na wabunge, pamoja na kubanwa huko, lakini wanapewa mawazo ya jinsi ya kutekeleza Bajeti zao. Wabunge wanapowabana mawaziri katika Bajeti wanaainisha maeneo ambayo yana matatizo. Hivyo waziri anapata ufahamu wa maeneo ambayo anapaswa kujikita wakati wa utekelezaji wa Bajeti yake.

Lakini hali haikuwa hivyo kwa Dk. Mpango kwa sababu wabunge wengi waliishia kumsifia kwa kuwasilisha Bajeti nzuri. Wengi walisifia uamuzi wa kufuta ada ya leseni ya kila mwaka ya barabara kwa magari. Baada ya hapo wakaanza kumsifia Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua kulinda maliasili za nchi hasa madini.

Wapinzani nao, ambao walitarajiwa wampe Dk. Mpango mawazo mbadala, wakajikuta wamekwama katika mtego wa kujibishana na wabunge wa CCM kuhusiana na ripoti ya makinikia. Kwa maana hiyo, kulikuwa na michango michache sana ya kuijenga hotuba ya Bajeti ya Dk. Mpango.

Mathalani, kulikuwa na hoja chache sana za mapendekezo ya nini Dk. Mpango na watu wake wafanye ili kuhakikisha nchi haikosi fedha zilizoahidiwa na wahisani kama sehemu ya Bajeti. Suala hilo ni muhimu kwa sababu Bajeti hii inayomalizika, utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni wa chini sana kwa sababu wafadhili hawakutoa fedha walizoahidi kupitia Bajeti.

Kwa maana hiyo, Dk. Mpango anaingia kwenye utekelezaji wa Bajeti ambayo kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unategemea fedha za wafadhili, wakati hajapatiwa maoni ya wabunge ni jinsi gani atapata fedha kutoka kwa wafadhili.

Kwa maana hiyo, Dk. Mpango inabidi akae chini mwenyewe na kuanza kufikiria jinsi ambavyo atawezesha nchi kupata fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili ili kutekeleza miradi ya maendeleo ili hali ya mwaka huu isijirudie mwakani.

Pole sana Dk. Mpango kwa sababu wabunge wamekuangusha. Pole kwa sababu ripoti ya bosi wako nayo imekuangusha lakini usimlaumu bosi wako kwa sababu alilolifanya amelifanya kwa manufaa ya Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles