KUJIFUNZA KUTOKA KWA WANAZUONI NI MUHIMU KATIKA UONGOZI

0
712
Mwanasheria Nguli wa Kenya, Profesa Patrick Lumumba

WIKI iliyopita Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kiliadhimisha Kongamano la Tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere. Hili ni kongamano maalumu ambalo hutumika kama uwanja wa kuchokoza mawazo na fikra mbalimbali kuhusu maendeleo ya Bara la Afrika. Katika makala haya NORA DAMIAN anaeleza yaliyojiri kwenye kongamano hilo.

MIAKA 18 baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, matendo na fikra zake bado zinaishi vichwani mwa watu.

Umuhimu wa Mwalimu si kwamba unaonekana sasa bali ulionekana tangu yungali hai, ndio maana alipofariki wengi walikuwa na mitazamo tofauti kwamba tutaweza kuishi bila Mwalimu…lakini tungali tunaishi.

Historia inatuonyesha kwamba Mwalimu alikuwa kiongozi mzalendo aliyeithibitishia dunia kujali utu na kuthamini wengine, mpigania haki na usawa kwa binadamu na kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi.

Alisisitiza maelewano, msamaha na upendo wa kweli kwa wote. Alipiga vita rushwa, ufisadi, ukabila, udini, hakuwa mroho wa madaraka,  alihimiza kujitegemea, alipenda umoja kati ya nchi na nchi mambo ambayo yanapaswa kuigwa na viongozi wa sasa.

Kwa vipimo vya ubinadamu ni wazi kuwa Mwalimu Nyerere aliitenda vema kazi aliyotumwa na Mungu.

Kila mwaka Kigoda cha Mwalimu Nyerere huwakutanisha watu wa kada mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kujadili masuala ya Bara la Afrika, kutoa mapendekezo, mikakati na kuangalia namna viongozi wenye dhamana wanavyoishi falsafa za Mwalimu.

Matamasha yanayoandaliwa na Kigoda hicho yamekuwa yakiibua mambo mengi ambayo kwa kiasi kikubwa yanalenga kuikomboa Afrika.

Washiriki wamekuwa wakipata nafasi ya kujadiliana na kueleweshana kwa uhuru na kila mchango uliokuwa ukitolewa uwe wa mshiriki wa kawaida, msomi ama mwanasiasa ulionekana kuthaminiwa.

Kongamano la mwaka huu lilijikita zaidi kumwangalia mwanasiasa namna anavyochangia kuinuka ama kuanguka kwa maendeleo ya Bara la Afrika ambapo wasomi mbalimbali walipata nafasi ya kutoa maoni yao.

Mijadala iliyotawala

Baadhi ya viongozi wastaafu, wasomi, wanataaluma mbalimbali na wasanii walipata nafasi ya kuchangia mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo.

Mzungumzaji ambaye alionekana kuvutiwa na washiriki wengi ni Mwanasheria Nguli wa Kenya, Prof.  Patrick Lumumba, ambaye alichambua udhaifu na mema ya viongozi kadhaa wa Afrika.

 

Prof. Lumumba ambaye alizungumza siku ya mwisho ya kongamano hilo alisema Waafrika wengi wanahitaji maendeleo yanayogusa maisha yao na si vingine.

“Mwafrika anataka chakula kizuri, shule, hospitali nzuri na ajira kwa vijana, tunataka viongozi watakaoboresha miundombinu, kilimo, maisha ya wanawake na watoto,” alisema Prof. Lumumba.

 

Alisema viongozi wengi wa Afrika wamekuwa wakiendesha siasa chafu, kujilimbikizia mali, wala rushwa, kutokuwa tayari kujisahihisha na kuendekeza ukabila.

 

“Hakuna siasa safi Afrika, kwa miaka 30 viongozi wanaotawala wamekuwa mafisadi na wabinafsi lakini mfumo unawapa fursa za kuendelea kuwa wachafu.

 

Nchi inaweza kujiita ya demokrasia kama Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) lakini haina demokrasia na leo hii ni kati ya nchi ambazo ni maskini,” alisema.

 

Alisema Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa na maono makubwa kwani aliipenda nchi yake na hata alipofanya makosa alitambua na kujisahihisha.

 

“Nyerere aliwahi kusema Ikulu ni mahali patakatifu lakini wako baadhi ya viongozi wakiondoka madarakani wanakuwa wamejilimbikizia mali na wengine hukutwa na mabilioni katika akaunti zao. Huyu ni mtu aliyewaunganisha watu wa makabila tofauti na kuwa taifa moja na kuzungumza lugha moja,” alisema Prof. Lumumba.

 

Prof.  Lumumba alisema kama ukabila hautapigwa vita utaendelea kuangamiza mataifa mengi na kutolea mifano ya nchi za DRC, Msumbiji, Zambia, Somalia, Nigeria, Kenya na Ethiopia.

 

“Suala la ukabila bado ni tatizo, Tanzania mna bahati kubwa kwa sababu Mwalimu Nyerere alijenga misingi imara ambayo inastahili kuigwa.

 

“Kenya ukijaribu kumuuliza mgombea atafanya nini pindi atakapochaguliwa anakwambia mimi ni Mluo na sasa ni zamu yetu, wengine unamuuliza rais wa awamu ya tatu ni nani anakujibu kuwa ni Uhuru na ni Mkikuyu tunataka aendelee kutawala…Mungu aisaidie nchi yangu,” alisema.

 

Mjadala mwingine ni ule wa ‘Mwanasiasa mwanamke na harakati za usawa wa kijinsia Afrika’ ambapo miongoni mwa wachangiaji walikuwa Spika (mstaafu) Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda, Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu (CCM) na Mbunge Mstaafu, Anna Abdallah (CCM).

Spika Makinda alisema, safari ya mwanamke katika harakati za uongozi bado ni ndefu na kwa wale wanaotaka kuingia ni lazima wapambane kwa kila mbinu na kuepuka kuonyesha udhaifu wao hadharani.

“Tuliposimama mwaka 1995 wakati vyama vingi vimeingia ilikuwa shughuli na baada ya hapo nilishtakiwa mahakamani kwa miaka minne watu wanapinga matokeo.

“Si rahisi wanawake kugombea lakini kama wameamua lazima wapambane kwa kila mbinu na kuepuka kuonyesha udhaifu wao hadharani,” alisema Makinda.

Dk. Nagu alisema wanaume hawawezi kumaliza changamoto peke yao na akawataka wakubali kushirikiana na wanawake.

“Wanaobeba umaskini wa Tanzania ni kinamama, hivyo tukubali kwamba wanawake lazima wawe sawa na wanaume. Mfumo dume ni pingamizi kwa mambo mengi, nilipokuwa Waziri wa Utumishi kama kuna nafasi za wakurugenzi ziko wazi walikuwa wanaleta majina ya wanaume tu, wanasema hakuna wanawake wenye sifa,” alisema Dk. Nagu.

Kwa upande wake Anna Abdallah, alisema katika ngazi za uamuzi wanawake wako wachache lakini wakitumia vizuri nafasi zao watawainua wenzao.

“Unapokuwa katika chombo cha uamuzi usikubali kusikia maneno ya kudhalilisha wanawake wenzako, mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa karibu miaka 20, wakati wa kupitisha majina mtu anasema mwanamke fulani hafai, ukiuliza sababu unajibiwa eti anapenda wanaume.

“Sikuona aibu niliwauliza mwanamume gani hapendi mwanamke…tukifika hapo wananyamaza kimya. Niliwaambia hiyo si sifa na tusipeane maneno ya kudhalilishana, tukikataa kule kwenye vyombo vya uamuzi wanawake watapita,” alisema Anna.

Naye Mwanamuziki Nikki wa Pili alisema; “Ukombozi wa Afrika hautaletwa na masihi, turudishe nguvu kwa wananchi na kutengeneza taasisi za kidemokrasia.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Relini, Agatha Venance, aliuliza swali katika kongamano hilo ‘Kwanini tamaduni nyingi za Afrika hazikubaliki na watu wa Afrika na badala yake huzikubali tamaduni za Magharibi?

Akijibu swali hilo, Msanii Kalola Kinasha, alisema suala hilo linatoka na kasumba mbaya iliyozoeleka kwamba ili uendelee ni lazima uige vitu vya Wazungu.

“Huhitaji kufanana na Mzungu ama Mchina, wote tuko tofauti na tumeumbwa hivyo kwa sababu. Tuachane na mikorogo sisi Waafrika ni wazuri sana,” alisema Kinasha.

Mkurugenzi wa Kituo cha Jinsia cha UDSM, Dk. Eugenia Kafanabo, ambaye alikuwa mmoja wa wenyeviti wa mijadala alisema; “Watoa mada wamefungua vichwa vyetu na wametupa elimu ambayo wengi tulikuwa hatuna, tutakwenda kuwaelimisha na wengine,” alisema Dk. Kafanabo.

Tamasha linawavutia wengi kutoka nje

 

Kadri miaka inavyosogea ndivyo tamasha hili linawavuta watu wengi kutoka nje ya Tanzania

Mchambuzi wa Siasa za Afrika, Dk. Kelvin Nyamori, ambaye kwa sasa anaishi Nigeria ni miongoni mwa watu waliovutiwa kuja kushiriki tamasha la mwaka huu.

Alisema; “Niliposikia kwamba kati ya wazungumzaji wa mwaka huu atakuwapo pia Prof. Lumumba, niliamua kusafiri kuja kumsikiliza.

Alisema dhana kwamba wananchi wana ndoto zao na viongozi wana matakwa yao ni tata na kwamba haiwezi kuifikisha nchi popote.

Mwanakigoda wa mwaka huu

Mwanasiasa na Mwanadiplomasia mkongwe kutoka Senegal, Prof.  Abdoulage Bathily ambaye ndiye alikuwa Mwanakigoda wa mwaka huu, alisema ni muhimu viongozi waasisi wakaenziwa kwa matendo yao.

Prof.  Bathily ambaye alishiriki katika mikutano mingi ya kutatua mizozo ya kisiasa Afrika, anasema mataifa yanayo wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima ya mtu aliyejitolea kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.

Mwenyekiti wa Kigoda

 

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Prof. Penina Mlama, alisema kongamano hilo limekuwa likisaidia kuenzi fikra za Mwalimu katika kuleta maendeleo kwenye nchi zinazoendelea.

Alisema awali jamii ilikuwa haimuenzi Mwalimu kutokana na fikra zake za ujamaa lakini hivi sasa imeanza kumwelewa na kufuata mambo mazuri aliyoyafanya.

Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Prof.  Rwekaza Mukandala, alisema baadhi ya viongozi wa Afrika wanachangia kuanguka kwa mataifa yao.

Jukwaa hilo la majadiliano na kitaaluma linayakumbusha mataifa kutambua kwamba kujifunza kutoka katika majadiliano ni muhimu zaidi kwa ustawi wa nchi.

Pamoja na pongezi kwa waandaaji wake ni muhimu kumkumbuka Mwalimu kwa matendo kwani hata katika utawala wake alionyesha njia kwa vitendo na alitaka wale wanaoongozwa wafuate njia hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here