LONDON, ENGLAND
KOCHA wa klabu ya Tottenham, Mauricio Pochettino, ameweka wazi kuwa upendo anaouonesha kwa mshambuliaji wake, Harry Kane, unamfanya agombane na mke wake.
Kocha huyo amesema ana upendo mkubwa kwa mshambuliaji huyo kutokana na kile anachokifanya uwanjani, lakini anashangazwa na mke wake kuchukia kwa yeye kumpenda mchezaji huyo.
Kane juzi alionesha kiwango cha hali ya juu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya mchezaji huyo kufunga mabao matatu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Apoel Nicosia, hivyo Pochettino alikuwa na furaha ya hali ya juu kumwona mchezaji huyo akifunga mabao.
“Ni wazi kwamba mke wangu anachukia sana kuniona nikionesha upendo wa dhati kwa mchezaji huyo, sijui hata kwanini, lakini najua ndivyo wanawake walivyo, hata mke wa Kane kuna wakati anachukia sana akiniona ninampenda mchezaji huyo, lakini wanatakiwa kujua kwamba mapenzi yangu kwa mchezaji huyo ni kutokana na kile anachokifanya uwanjani.
“Siwezi kumchukia au kuacha kumpenda kutokana na wake zetu, mchezaji huyo anafanya kile ambacho mashabiki wa soka wa Tottenham wanapenda kukiona uwanjani,” alisema Pochettino.
Kane mwenye umri wa miaka 24, kwa sasa ana jumla ya mabao 11 katika michezo saba aliyocheza ndani ya klabu hiyo na timu ya Taifa, wakati huo mwaka 2017 amecheza jumla ya michezo 30 na kufunga mabao 34 ndani ya klabu.
Mchezaji huyo ameingia kwenye historia ya kufunga mabao ya ‘hat trick’ kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa wachezaji wa nchini England, akiwa ni mchezaji wa saba baada ya Andy Cole, Mike Newell, Michael Owen, Wayne Rooney, Alan Shearer na Danny Welbeck.
Mbali na Tottenham kushinda katika mchezo huo wa juzi, michezo mingine ambayo ilipigwa siku hiyo ni pamoja na Real Madrid wakiwa ugenini walifanikiwa kushinda mabao 3-1 dhidi ya Borussia Dortmund, Napoli ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Feyenoord, huku Besiktas ikishinda 2-0 dhidi ya RB Leipzig, Shakhtar Donetsk wakipigwa 2-0 dhidi ya Man City, Sevilla ilishinda 3-0 dhidi ya Maribor, wakati huo Spartak Moskva wakitoka sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool na Monaco ikipigwa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Porto.