24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm ndio basi tena Yanga

KOCHA mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm
KOCHA mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, yuko katika hatari ya kutimuliwa katika timu hiyo kutokana na mwenendo wa kikosi hicho katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.

Pluijm ambaye amejiunga na Yanga takribani misimu mitatu iliyopita na kuipa mafanikio ya kutwaa Kombe la Shirikisho la TFF (FA), Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara na kuifikishia Yanga kwa mara ya kwanza katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Taarifa ambazo MTANZANIA Jumapili linazo zinasema kuwa licha ya kocha huyo kurejea kukinoa kikosi hicho baada ya kuandika barua ya kujiuzulu hivi karibuni, bado viongozi wa juu wameshikilia msimamo wa kumwondoa kwenye nafasi hiyo.

Imeelezwa kuwa kutokana na matokeo yasiyoridhisha kumekuwa na maswali mengi kwa uongozi ikiwemo nini sababu ya kupata matokeo hayo wakati mahitaji yote muhimu ambayo benchi la ufundi limekuwa likihitaji yanatimizwa kwa wakati.

“Laiti kama Pluijm angejua yanayomjia mbele yake, ni heri angeshikilia msimamo wa kujiuzulu kuliko kukubali kuifundisha Yanga na kuja kuachwa kwa aibu,” alisema mtoa habari huyo ndani ya klabu hiyo.

Alisema hivi sasa linaundwa zengwe juu ya kwanini wachezaji wengine aliowataka mwenyewe wasajiliwe anashindwa kuwapa nafasi wakati Yanga inaendelea kuwalipa mishahara na kuingia hasara.

“Yapo mengi ambayo yanasababisha Pluijm kutoendelea kuwepo Yanga kwani hata hiyo nafasi ya ukurugenzi wa ufundi iliyodaiwa atapewa upo uwezekano asiwekwe, kwani tayari imeshakuja hisia mbaya kuwa anaweza akashauri vibaya.

“Hivi sasa kinachosubiriwa ni timu kurejea Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mechi yetu na Tanzania Prisons, ili uongozi wa juu ukutane na Pluijm na kujua nini sababu ya klabu  kuchukua maamuzi ya kuvunja naye mkataba na kumkabidhi majukumu kocha mpya atakayetua nchini muda wowote kuanzia Jumapili,” alisema.

Sakata la kung’olewa kwenye nafasi ya ukocha kwa Pluijm, lilianza mwezi uliopita baada ya kudaiwa kuwepo kwa mazungumzo baina ya Yanga na kocha Geogre Lwandamina ambaye ni kocha wa Zesco ya Zambia na huenda akawasili jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya kumalizana na Yanga. Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakupatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles