
Hospitali ya Kairuki katika kuboresha huduma zake kwa wagonjwa imeanza kutumia kitengo kipya kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa kutwa hususani wale wanachama wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, NHIF.
Kwa mujibu wa Afisa uhusiano wa hospitali hiyo, Arafa Juba, kitengo hicho kipya (OPD 3) kilichopo nyuma ya Jengo kuu la hospitali mkabala na kitengo cha magonjwa ya viungo (Physiotherapy Unit), kina sehemu kubwa ya mapokezi, vyumba mbalimbali vikiwemo vyumba 10 vya madaktari, maabara, duka la dawa, sehemu ya sindano na kufunga vidonda, chumba cha ultrasound, mapokezi , huduma za chanjo ya watoto (RCH), chumba cha wauguzi na duka dogo la vinywaji na vitafunwa.
“Kitengo hicho kipya kitaiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma kwa haraka na ufanisi zaidi kwa wagonjwa wasiopungua 120,000 kwa mwaka hivyo kupunguza kero ya foleni na msongamano uliokuwepo siku za nyuma,” alisema Juba.
Juba aliongeza kuwa kitengo hicho (OPD3) kitazinduliwa rasmi hivi karibuni pamoja na vitengo vipya vya kusafishia figo ( Dialysis Unit) na cha huduma za dharula ( Emergency Unit).