NA JUMA KASESA, TUNISIA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Der Plujim, ameapa kuiandikia historia timu hiyo kwa kuitoa timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Yanga iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa awali uliopigwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, leo inavaana na timu hiyo katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza utakaofanyika katika Uwanja wa Olimpique de Sousse utakaoanza saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Akizungumza mjini hapa, Pluijm alisema vitimbi vya Waarabu hao havitawazuia wasipate kipigo na kwamba wachezaji wake wamemhakikishia kuwa hawajaathiriwa na vitendo walivyofanyiwa kwa kugandishwa kwa saa mbili pasipo kugongewa viza.
Alisema amewaandaa nyota wake kuishambulia ngome ya Etoile katika dakika zote za mchezo ili kupata bao la faida ili kuwachanganya wenyeji wao kabla ya kutafuta jingine la ushindi ili kujiweka salama.
Mara baada ya kutua juzi mchana na kufikia katika hoteli ya kitalii ya El Mourad Palm Marina, walifanya mazoezi mepesi ya nusu saa usiku katika Uwanja mdogo wa Etoile uliopo kilomita 10 kutoka katika hoteli hiyo na jana walifanya mazoezi katika Uwanja wa Olimpique de Sousse, utakaochezwa mchezo huo.
Yanga jana jioni ilifanya mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa wa upinzani mkali huku nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akisema wamekuja Tunisia kuandika historia kwa kuiondoa timu hiyo.
‬Etoile inaelezwa wamekuwa na mchecheto baada ya kupata taarifa kuwa Yanga wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.