Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM
KOCHA wa Yanga, Hans Van der Pluijm, ametajwa kuhitajiwa na klabu moja nchini Misri, baada ya kumalizana na uongozi wa wanajangwani.
Pluijm kwa sasa ataondoka Yanga kutokana na uongozi wa klabu hiyo kuingia mkataba wa miaka miwili na kocha Mzambia, George Lwandamina ambaye tayari yupo nchini.
Habari za kuaminika zilieleza kuwa tayari timu hiyo kubwa nchini Misri, imeonyesha nia ya kumchukua Pluijm.
Chanzo cha habari kilisema kuwa, mara baada ya Yanga kumalizana na Pluijm, Mholanzi huyo ataelekea Misri kuanza kibarua kipya katika klabu hiyo.
“Pluijm ameanza kupata ofa kutoka katika klabu mbalimbali, lakini hadi sasa taarifa za uhakika ni kuwa mazungumzo kati yake na klabu hiyo ya Misri yanaendelea,” kilisema chanzo hicho.
MTANZANIA lilipomtafuta kocha huyo kuzungumzia suala hilo, alisema kuwa hayupo tayari kusema kitu chochote kwa sasa.
“Sipo tayari kuzungumzia jambo hilo kwa sasa, muda utakapofika kila kitu kitakuwa hadharani na ukweli utajulikana,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo aliwasilisha barua ya kujiuzulu kufundisha timu hiyo mwezi uliopita, lakini alirejea na kuendelea na majukumu yake baada ya mazungumzo ya siku tatu na mwanachama wa klabu hiyo, Mwigulu Nchemba.