28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm achoka na uteja Yanga

NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van Der Pluijm, amesema kama ataendelea kukinoa kikosi hicho, anaamini atafuta uteja wa kufungwa na watani wao wa jadi, Simba, ambao mara yao ya mwisho kuwafunga katika ligi ilikuwa msimu wa 2012/ 2013.
Yanga, ikiwa inanolewa na kocha Mholanzi, Ernest Brandts, iliibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Simba Mei 19, 2013, huku Wanajangwani hao wakiweza kuibuka mabingwa wa msimu huo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, baada ya kufungwa bao 1-0 na wekundu hao wa msimbazi, Pluijim alisema matokeo ya kushindwa kufanya vizuri kila wanapokutana na Simba yanakaribia kumalizika, kwani mara kadhaa wanapokutana mbali na mechi za ligi wamekuwa wakifungwa.
“Tutamaliza hili suala la kufungwa, kila kitu kinahitaji muda, hii ni mara yangu ya pili kukiongoza kikosi changu kuvaana na Simba, katika mchezo wetu wa mzunguko wa pili, msimu wa 2013/2014 tulitoka sare bila kufungana,” alisema Pluijm.
Alisema wakati anakabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa Brandts, ambaye alitimuliwa na uongozi kutokana na matokeo mabovu, aliweza kuwadhibiti Simba.
Mbali na kauli yake hiyo, Pluijm alimzungumzia mchezaji Emmanuel Okwi kuwa ni mchezaji hatari na wa kuogopwa.
“Okwi ni mchezaji hatari, kwani anaweza kubadilisha matokeo wakati wowote, ogopa mchezaji kama huyo,” alisema.

Alieleza katika mchezo wa juzi aliamua kumtoa Danny Mrwanda, ili kuepusha ugomvi, kwani tayari mchezaji huyo alionyesha kuwa tatizo uwanjani.
“Nilimtoa Mrwanda nikiwa na maana yangu, hakuwa vizuri kabisa, nililiona hilo, nilichokifanya ni kumwepushia kadi nyekundu, alionekana kuwa na jazba,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alikwenda mbali zaidi na kusema tukio la mchezaji wake, Haruna Niyonzima kupewa kadi nyekundu limemuumiza sana na litamlazimu kufanya mazungumzo ya kina kufahamu ukweli kutoka kwa kiungo huyo.
Wakati huo huo, Niyonzima alipozungumza na gazeti hili, aliwatupia lawama mashabiki na kudai wao ndio waliosababisha apewe kadi kutokana na makelele yaliyopelekea ashindwe kusikia mlio wa filimbi.
“Sina kosa lolote mimi, unajua zile kelele za mashabiki bwana kila mtu anaongea lake, wakati ule unakuta na sisi wachezaji vichwa vinawaza mabao,” alisema Niyonzima.
Upande wa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema hakuna haja ya mabeki wao kulaumiwa, kwani walionyesha kiwango kizuri, ila bao alilofunga Emmanuel Okwi lilikuwa bora zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles