27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm aanika kilichoiua Mwadui

Hans van der PluijmNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema aliwaandaa kisaikolojia wachezaji wake kuhakikisha wanacheza kwa ushirikiano uwanjani dhidi ya Mwadui FC huku wakitambua matokeo ya ushindi ni muhimu kwa timu hiyo.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, alilazimika kuongeza mbinu za kuwapa wachezaji wake kipindi hiki cha mechi za lala salama kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na ushindani uliopo katika mbio za kuwania ubingwa.

Yanga juzi ilifanikiwa kuichapa Mwadui ya Shinyanga mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuzidi kuwafukuzia mahasimu hao Simba wanaoshika usukani wa ligi hiyo.

Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 57 kutokana na michezo 24 waliyocheza wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 56 baada ya kushuka dimbani mara 23.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Pluijm alielezea kufurahishwa na ushindi waliopata licha ya kikosi chake kufanya makosa madogo madogo ambayo yangeweza kuwagharimu na kupoteza pointi muhimu.

“Soka ni mchezo wa makosa hivyo wachezaji kukosea ni jambo lisiloweza kuzuilika, pointi tulizopata zimetuongezea nguvu kwani matokeo ya ushindi yalikuwa ni muhimu sana kwa upande wetu,” alisema.

Kocha huyo ambaye pia kikosi chake kinakabiliwa na mchezo wa hatua ya 16 bora ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, alisema wachezaji walishindwa kuzitumia nafasi nyingi walizotengeneza kipindi cha kwanza huku akidai kiwango kiliongezeka waliporejea uwanjani kipindi cha pili.

“Wachezaji walicheza kwa kujiamini zaidi hasa kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi saba za kufunga lakini wakapata bao moja, kuna makosa katika umaliziaji hali ambayo ni lazima ifanyiwe marekebisho haraka,” alisema.

Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka  keshokutwa kuelekea nchini Misri kwa maandalizi ya mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaochezwa Aprili 20, mwaka huu jijini Cairo, Misri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles