28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda ahimiza uzalishaji wa mbogamboga Afrika kuondoa utapiamlo

Na Janeth Mushi, Arusha

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo katika Bara la Afrika wakiwemo serikali na sekta binafsi kuhakikisha uzalishaji mkubwa wa mazao ya mbogamboga unafanyika katika maeneo yao ili kupunguza tatizo la utapiamlo Afrika.

Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Agri Thamani Foundation, ametoa kauli hiyo leo Januari 25, wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa kujadili mazao ya mbogamboga yenye asili ya Afrika “All-Africa Summit on Diverstifying food systems with African traditional vegetables to increase health,nutrition and wealth”.

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akiwa kwenye mkutano huo.

Amesema mkutano huo ni muhimu kwa washiriki wote hasa wazawa wa Bara la Afrika katika kuangazia mazao ya mbogamboga yenye asili ya bara hilo na kuwa siyo kuangazia lishe na kipato tu bali utamaduni na ustawi.

“Kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya mazao ya mbogamboga yenye asili la kiafrika si kazi ya serikali tu bali wadau wote wakiwemo watafiti, wakulima, wafanyabiashara katika sekta ya usafirishaji, uuzaji wa mazao ghafi na usindikaji.Natoa wito kwa wadau wote kuhakikisha mazao haya yanapewa kipaumbele,” amesema Pinda.

Amesema Afrika inayo zaidi ya aina 800 za mazao ya mboga za asili lakini yanayotumika kama chakula ni machache sana huku yanayotumika kibiashara yakiwa machache zaidi.

“Huu ni urithi wetu wa mazao hivyo ni lazima tuutunze na kuuenzi ikiwemo kutunza bioanuai yetu isipotee kwani utafiti unaonyesha kutokana na kutokufanyiwa utafiti wa kutosha na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi mimea ya mbogamboga hasa ile ambayo hailimwi inazidi kupotea kwa kasi.

“Mazao ya mboga ni muhimu sana kwenye afya na lishe,utafiti wa kitaalam unaonyesha kuwa mboga za asili zina viwango vikubwa vya viini lishe ukilinganisha na mboga nyingine kutoka mataifa ya nje ya Bara hili,kufuatana na takwimu za FAO kuna watu milioni 821 wanakabiliwa na matatizo ya utapiamlo yanayotokana na chakula kisichokuwa na viinilishe,” amesema Pinda.

Sehemu ya Washiriki wa Mkutano huo

Amesema kwa upande wa Tanzania hali ya utapiamlo ni mbaya na kulingana na takwimu za utafiti wa hali ya lishe ya mwaka 2018 zinaonyesha watoto milioni tatu wenye umri wa (miaka 0-5) wamedumaa, watoto milioni 1.3 (miaka 0-5) wana uzito pungufu, watoto milioni tano wenye umri huo wana upungufu wa damu huku milioni tatu wakiwa na upungufu wa Vitamini A na asilimia 32 ya wanawake (miaka 14-49) wana tatizo la uzito uliozidi.

“Baadhi ya athari za utapiamlo ni pamoja na udumavu ambao una athari katika makuzi ya maendeleo ya maendeleo ya mtoto,utapiamlo unaongeza magonjwa na vifo kwa watoto na akina mama,upungufu wa damu pia huathiri uwezo wa kujifunza na utendaji kazi kwa asilimia 17.

“Ili kupambana na tatizo hilo kwa akina mama kwa makadirio ya mwaka 2019 serikali ilipanga kununua vidonge milioni 179.2 ili kukidhi mahitaji ya vidonge vya kuongeza damu kwa wajawazito na viligharimu Sh bilioni 3.3,” amesema Pinda.

Ameongeza kuwa upo umuhimu mkubwa kwa Tanzania kudhibiti tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka  mitano na kuwa mazao ya mbogamboga ni fursa kubwa kibiashara katika ngazi ya kaya hadi taifa.

Akizungumzia kuhusu mchango wa Agri Thamani Foundation katika kuhamasisha hilo wameanzisha elimu lishe na kuanzisha bustani za mfano katika shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika mikoa saba.

Amesema wameanzisha bustani za mfano kwenye shule hizo, kaya zenye watoto chini ya umri wa miaka  mitano na wenye uhitaji mkubwa wa lishe, zoezi ambalo limeanza mwishoni mwa mwaka jana.
 
“Kanda ya ziwa kule tumetumia muda mwingi kwani tulichogundua mkoa wa Kagera,ukiangalia takwimu zake za utapiamlo mambo ni mazuri lakini unapokwenda kwenye uhalisia wa takwimu unakuta idadi ya watoto wanaooumia Kagera ni kubwa,tumeweka nguvu kubwa na tumeanzisha miradi  kwenye shule,” amesema Pinda.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Kituo cha Utafiti wa mbogamboga na matunda cha Kimataifa cha World Vegetable Center, Dk Gabriel Rugalema, ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo amesema lengo ni kujadili hatima ya mazao ya mbogamboga yenye asili ya Afrika.

Meza Kuu

Amesema katika mkutano huo wa siku tatu unaofanyika jijini hapa umeshirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu,walimu wa vyuo vikuu,watafiti kutoka vyuo vya kitaifa na kimataifa,wafanyabiashara na wadau wengine.

“Tmeitisha mkutano huu kwa sababu mazo yetu ya mbogamboga za asili yako kwenye hatari ya kutoweka na kupotea na vilevile umuhimu wake katika mifumo ya chakula hapa barani Afrika, tutajadiliana,kuhamasisha na kujenga mkakati wa kuwezesha ongezeko la utafiti, uwekezaji, uzalishaji na matumizi bora ya mazao ya mbogamboga asilia,”amesema Dk. Rugalema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles