KOCHA wa Manchester City, Manuel Pellegrini, ameanza kuwaaga wachezaji wake mara baada ya kocha mtarajiwa, Pep Guardiola, kusaini mkataba wa miaka mitatu.
Guardiola amesaini mkataba huo mwanzoni mwa wiki hii ambapo kazi ataanza kuifanya
Julai mosi baada ya Pellegrini kumaliza mkataba wake Juni 30 mwaka huu.
Hata hivyo, Pellegrini alikutana na wachezaji wake kabla ya mchezo wa juzi na kuwaambia kwamba ‘alijua tangu miezi iliyopita kama Guardiola atakuja kuchukua nafasi hiyo.’
“Ningependa kutumia nafasi hii kuongea na nyinyi wachezaji wangu, najua kila mmoja anajua nini kitakachotokea lakini kwa upande wangu nilijua mapema, lakini kwenu labda kimewashtua.
“Ukweli ni kwamba, nitaondoka Juni 30 mwaka huu na kumpisha mwenzangu Guardiola ambaye amesaini
mkataba wa miaka mitatu, kikubwa ni kumpa heshima yeka na kufanya naye kazi vizuri ili kuleta ubingwa.
“Kwa sasa kinachotakiwa ni kujituma kwa hali ya juu kuhakikisha tunachukua ubingwa wa ligi na Ligi ya
Mabingwa na mataji mengine ili kuweza kumpa nafasi nzuri kocha ajaye,” alisema Pellegrini.
Hata hivyo, kocha huyo amedai kwamba lengo lake kubwa ni kuendelea kuwa kocha katika klabu za England mara
baada ya kuondoka Man City.