RABAT, Morocco
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Fransis, amesema mji wa Jerusalem unapaswa kuwa ishara ya amani ya kuishi pamoja kwa jamii za Wakristo, Wayahudi na Waislamu.
Kwenye taarifa yao pamoja iliyotolewa na Papa Francis na Mfalme Mohamed VI wa Moroco mjini hapa jana, viongozi hao wawili walisema mji wa Jerusalem umekuwa eneo la urithi wa pamoja kwa binadamu na zaidi kwa waumini wa hizo dini tatu.
Papa Francis na Mfalme Mohamed wametaka kulindwa na kuenziwa kwa sifa za mji wa Jerusalem ikiwamo torati na majengo yenye kuonyesha mchanganyiko wa iimani.
Tamko hilo la pamoja limetolewa baada ya tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuitambua Jerusalem eneo linalozozaniwa kuwa mji mkuu wa Israel.
Uamuzi huo umezusha ghadhabu kwa waislamu hususan kutoka Palestina wanaouzingatia mji huo kuwa makao makuu ya taifa lao la siku zijazo.
Katika ziara yake hiyo, Baba Mtakatifu pia alikutana na wahamiaji na viongozi wa kiislam na akaendesha ibada katika taifa hilo lenye idadi ndogo ya waumini wa Kanisa Katoliki.
Katika hotuba yake wakati wa ibada hiyo, Papa Fransis aliwahimiza waumini wa dhehebu hilo kushirikina na mengine kupinga vitendo vya ubaguzi wa imani na akawataka kuishi kama ndugu.