VATICAN, ITALIA
MMOJA wa wakosoaji wakubwa wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema kauli yake ya hivi karibuni kuhusu wapenzi wa jinsia moja ni maoni binafsi ambayo hayastahili kuzingatiwa na Wakatoliki.
Kadinali Raymond Burke anayeonekana kuwa mhafidhina katika Kanisa Katoliki, ametoa tamko hilo siku chache baada ya Papa Francis kuonekana kuunga mkono wazo la kutambuliwa kisheria kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Kadinali Burke anasema pendekezo la Papa Francis la kutaka ndoa ya wapenzi wa jinsia moja kutambuliwa kisheria halijawashangaza wengi lakini maneno aliyotumia ndio yaliyowashangaza sana viongozi wa kidini na waumini wa Kanisa Katoliki.
Kadinali huyo ametaja matamshi ya Papa kama maoni ya kibinafsi na kwamba Kanisa katoliki na waumini wake hawatashurutishwa kutii msimamo wa kiongozi wa Kanisa hilo kuhusu suala la wapenzi wa jinsia moja.
Pia amesema viongozi wa kidini wa kanisa hilo wana jukumu la kutoa kile alichokitaja kama maelezo ya kina kuhusu suala hilo.
Kadinali Burke amesema imani rasmi ya kanisa Katoliki la Roma ni kuwa ndoa ya wapenzi wa jinsia moja hairuhisiwi na kwamba matamshi hayo ya papa yamewahuzunisha waumini wengi akidai kuwa hayaambatani na mafundisho ya Kanisa hilo.
Suala la ndoa ya wapenzi wa jinsia moja limekuwa na utata katika kanisa katoliki
Chini ya mafundisho ya sasa ya Katoliki, uhusiano wa wapenzi wajinsia moja unaangaziwa kama tabia potofu.
Lakini Papa Francis alisema anafikiria wapenzi wa jinsia wanastahili kuruhusiwa kuoana.
“Watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wana haki ya kuwa na familia,”alisema katika filamu, ambayo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatano wiki hii.”
“Ni watoto wa Mungu na wana haki ya kuwa na familia. Hakuna mtu anayestahili kutengwa ama kufanywa ajihisi mnyonge kwa kuamua kuwa katika uhusiano wa aina hiyo.
“Tunachopaswa kuunda ni sheria ya kutambua uhusiano wao ili kuwalinda kisheria.”
Aliongeza kwamba “aliunga mkono wazo hilo”, akiashiria nyakati alipokuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, akisema japo alipinga ndoa ya wapenzi wa jinsia moja, aliunga mkono ulinzi wa kisheria kwa watu walio kwenye mahusiano ya kama hayo.
Filamu ya Francesco, inayoangazia maisha na kazi ya Papa Francis, ilionyeshwa kama sehemu ya Tamasha la Filamu la Roma.
Lakini kile kilichosalia katika vinywa vya watu wengi ni msimamo rasmi wa Kanisa Katoliki kuhusiana na suala hilo.
“Kitu alichosema Papa Francis bilashaka sio jambo geni katika Kanisa Katoliki. Ni suala ambalo limekuwa likitiliwa mkazo katika miaka ya hivi karibuni ,”Mwanathiolojia Massimo Faggioli ambaye pia aliandika kitabu cha Papa Francis.
Papa Francis aliwahi kusema: Kanisa linastahili kuwaomba msamaha wapenzi wa jinsia moja.
Mafundisho ya Ukatoliki na Kanisa Katoliki ambayo, ambayo yaliyoandikwa kando kando kwa karne kadhaa, yalichapishwa kikamilifu mwaka 1997 na John Paul II na kufanyiwa mabadiliko na Benedict 16 mwaka 2005.
Sasa, mafundisho haya yanaweza kurekebishwa na Papa kupitia kongamano maalum la waumini.
Mfano wa hivi karibuni marekebisho mafundisho hayo yalifanywa na Papa Francis mwenyewe mwaka 2018 ni ya kutangaza adhabu ya kifo “haikubaliki” na pamoja na kujitolea kuipigania ulimwenguni.
Wachambuzi wanakubaliana kuwa matamshi ya Papa Francis hayakuidhinisha ndoa ya wapenzi wa jinsia moja.
“Kwa msingi huo, msimamo wa Kanisa haujabadilika,” anasema Faggioli.
Tofauti na watangulizi wake, Papa Francis ameamua kuonesha moyo wa huruma kwa wapenzi wa jinsia moja katika jamii tangu alipochukua hatamu ya uongozi mwaka 2013, jambo ambalo limemfanya kukosolewana viongozi wahafidhina wa Vatican.
Pia amelaumiwa kwa na baadhi ya watu kuwa ni “mnafiki: kwa kutoa matamshi bila kufanya mabadiliko yoyote.
Mwaka 2013, katika kitabu cha Heaven and Earth, Papa alisema kuwa kusawazisha kisheria mahusiano ya jinsia moja na ndoa za jinsia moja itakuwa “upungufu wa kianthropolojia”.
Pia alisema ikiwa wanandoa wa jinsia moja wataruhusiwa kuasili, “watoto huenda wakaathirika … kwani kila mtu anahitaji kuwa na baba wa kiume na mama wa kike ambao wanaweza kuwasaidia utambulisho wao”.
Mwaka huo huo,alisisitiza msimamo wa Kanisa kwamba vitendo vya ushoga ni dhambi, lakini akasema mwelekeo wa ushoga sio.
“Ikiwa mtu anashiriki mapenzi ya jinsia moja na anamtafuta Mungu kwa nia njema, mimi ni nani nimhukumu?,”aliuliza.
Mwaka 2014 iliripotiwa kuwa Papa Francis aliashiria kuunga mkono ndoa ya wapenzi wa wa jinsia moja katika mahojiano, lakini ofisi yake ya mawasiliano ilikanusha taarifa hizo.
Mwaka 2018, Papa Francis alisema “ana hofu” kuhusu mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa makasisi akiongeza kwamba ni “jambo zito”.