Na Waandishi Wetu
GENGE la vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam linalofahamika zaidi kwa jina la Panya Road, jana usiku lilivamia maeneo mbalimbali ya jiji na kufanya vitendo vya uhalifu.
Taarifa za kufanyika kwa vitendo hivyo vya uhalifu zilifika katika chumba cha habari cha gazeti la MTANZANIA Jumamosi saa 2.00 usiku na dakika chache baadaye zilisambaa katika mitandao ya kijamii huku zikiwa zimebeba ujumbe unaowatadharisha watu kutotoka nje ya nyumba zao.
Jirani na ofisi za gazeti hili, watu walikuwa wakikimbia hovyo baada ya milio ya risasi kusikika kutoka eneo la Sinza Whiteinn.
Baadhi ya mashuhuda wa matukio hayo waliozungumza na gazeti hili kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji kwa njia ya simu walieleza kuwa kundi la vijana hao lilianza kushambulia raia na kuwapora mali zao katika eneo la Magomeni.
Mashuhuda hao walisema vijana hao wakiwa katika eneo hilo la magomeni, walikabiliana na polisi na kuwalazimu kukimbilia eneo la Tandale huku idadi yao ikizidi kuongezeka.
Katika kipindi kisichozidi dakika 30 kundi la kihalifu la vijana hao lilikuwa limekwishasambaa katika maeneo ya Sinza, Kinondoni, Magomeni, Ubungo External, Mabibo na Mazense na Kijitonyama karibu mahali ziliko ofisi za usalama huku likipora na kuacha vilio kwa watu liliowajeruhi.
Mmoja wa mashuhuda hao, alilieleza gazeti hili kundi la vijana hao ambao msingi wa vurugu zao inasemekana ni kuuawa kwa mwenzao juzi, lilikuwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga, nyembe, marungu, visu, nongo na bisibisi.
Hali ilizidi kuwa ya mashaka zaidi ilipotimu majira ya saa 2.30 usiku baada ya chumba cha habari cha gazeti hili kuanza kupokea simu mfululizo zikielezea jinsi kundi la vijana hao lilivyokuwa likitekeleza vitendo vya kinyama huku polisi wakionekana kushindwa kulidhibiti.
Taarifa kutoka kituo cha polisi cha Oysterbay zilieleza kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokadiriwa kufikia zaidi ya 60 waliokimbilia kituoni hapo kuomba hifadhi kutokana na hofu ya kushambuliwa na genge hilo.
Mhariri wa Habari wa Gazeti la Mtanzania, Bakari Kimwanga ambaye alikutana genge la vijana hao eneo la Baa ya Whiteinn lililo karibu na Hotel ya Vatican, Sinza, alisema akiwa kwenye gari akirejea nyumbani aliona kundi la watu likikimbia kwa miguu huku likiwa limeshika mapanga, marungu na silaha nyingine za jadi.
Bakari alisema dereva wa gari lake alitoa kichwa nje ya kuwauliza watu waliokuwa wakilikimbia kundi hilo kitu kilichotokea na kujibu kuwa genge la uhalifu la Panya Road linashambulia raia na kupora mali.
Alisema baada ya kupewa taarifa hiyo, dreva huyo aligeuza gari kurudi eneo la Sinza kijiweni huku abiria wakiwa wanashuka na kukimbia hovyo.
“Mie niliingia Hospitali ya Palestina kujificha, nikiwa hospitali mama akanipigia akaniambia nyumbani maeneo ya Mwembechai hakufai Panya Road wamevamia.
“Hapo Hospitali tulikimbilia watu wengi na muda kidogo tukaanza kuona magari ya polisi yakipita kwa kasi kuelekea eneo la Sinza shekilango,” alisema Kimwanga.
Akielezea zaidi alisema wakiwa bado ndani ya eneo hilo walimshuhudia mwanajeshi mmoja akikikimbia barabarani huku akipiga filimbi ya kuashiria hatari.
Taarifa zaidi zilizokusanywa na gazeti hili polisi zilieleza kuwa taarifa za genge hilo kuanza kufanya uhalifu zilianza kusambaa kwenye vituo vya polisi majira ya saa moja usiku na kisha kwenye ujumbe kupitia mitandao ya whatsupp na mara moja polisi walitawanyika maeneo mbalimbali ya jiji ili kukabiliana nao.
Alipotafutwa msemaji wa jeshi la polisi nchini, Advera senso alikiri kusikia tukio hilo lakini akamtaka mwandishi wa gazeti hili kuwatafuta makamandama wa polisi wa mikoa ya Kinondoni, Temeke na Ilala ili kuzungumzia hali hiyo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, simu yake iliita bila majibu na hata alipopatikana baadae alikana kuwepo kwa taarifa za genge la panya road kuteka maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam.
“Hakuna kitu kinachoitwa Panya Road, huo ni uvumi tu, wananchi walikuwa wanavumisha” alisema Wambura.
Mwandishi wa habari hizi alipomwambia kwamba yeye alikuwepo maeneo ya Sinza zilipo ofisi za gazeti hili na alishuhudia polisi wakipiga risasi hewani mara mbili kutawanya vijana hao, Wambura bado alisisitiza kuwa huo ni uvuni.
Alipobanwa kueleza msingi wa polisi kufyatua risasi hewani ni nini ilihali hakuna tukio la panya road kuteka maeneo hayo alisema; “Sikiliza ninachokwambia mimi, kwani unafikiri mimi ni daktari hicho ninachokwambia ndio ukweli, bwana ninapokea taarifa nyingi hapa kama hutaki kukubali hilo basi” alisema Wambura na kisha kukata simu.
Wakati Kamanda Wambura akikanusha genge la Panya Road kuteka baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, alilieleza gazeti hili kupitia simu yake kiganjani kuwa makamishna wa Polisi walikuwa wanakutana kwa dharura kwa ajili ya kulichukulia hatua jambo hilo na katika kikao hicho walimuagiza Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kwenda kwenye vyombo vya habari kulizungumzia.