29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Membe, January wahofia urais

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

Bakari Kimwanga na Asifiwe George, Dar es Salaam
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe na January Makamba ambao wametangazi nia ya kugombea urais mwaka huu, wameanza kuonesha hofu kuhusu nafasi hiyo ya juu nchini.
Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Makamba ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekonolojia, wamepatwa na wasi wasi kutokana na uwepo wa taarifa za matumizi makubwa ya fedha katika kusaka nafasi hiyo.
Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam jana, Membe alisema taifa linakabiliwa na mambo mawili hatari ambayo ni rushwa na mmomonyoko wa maadili.
Alisema wapo watu wenye fedha nyingi ambao wana uwezo wa kununua mtu yeyote ili kufanikisha mipango yao ya kuingia madarakani, jambo ambalo halikubaliki.
“Wapo watu wenye fedha nyingi ambao wana uwezo wa kununu mtu yoyote…jambo hili ni hatari,” alisema.
Licha ya kutofafanua kauli yake, Waziri Membe aliwatahadharisha vijana kuwa makini na watu wa aina hiyo.
Alisema watu hao, wamekuwa wakiwarubuni kwa kutoa fedha ili wapate kile wanachokihitaji.
“Sasa ni wakati wa sisi Serikali kuomba msamaha kwa yale tuliyokosea kwa viongozi wa dini na kwa wananchi kwa ujumla ni vizuri tukatambua makosa ili tusiyarudie tena.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa la Anglikana na madhehebu mengine kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema Membe.
Alisema taifa linapita katika kipindi cha majaribu makubwa na mitihani mikubwa kutokana na kuwapo mmomonyoko wa maadili katika ngazi zote kuanzia ngazi ya familia, shule, ofisi na serikalini.
Alisema tatizo la rushwa, mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi ( albino), umasikini na tatizo la kupoteza uvumilivu wa kidini na kisiasa, vimechangia taifa kuporomoka.
Alisema Watanzania wengi wameanza kukata tamaa na kupoteza matumaini, jambo ambalo linaonekana kuwa changamoto kubwa kwa viongoi wa dini zote.
Alisema waumini wamekata tamaa na kupoteza hofu ya Mungu, huku watu wengine wamekuwa wakimbilia katika nguvu za giza, uganga na unajimu.
“Tunahitaji kutoka hapa, ni jambo la kujiuliza tunatokaje? Naamini kwa dhati watu wakishika mafundisho ya dini, wakamuogopa Mwenyezi Mungu, maovu mengi yatapungua, hayawezi kuisha, lakini yatapungua kwa kiasi kikubwa.
“Ninyi viongozi wa dini mnayo nafasi ya pekee kwa vile mnasikilizwa na waumini wenu, maneno yenu yanapokelewa vizuri kuliko wanasiasa au watu wengine,” alisema Waziri Membe.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Askofu Valentine Mokiwa alisema vijana wamekosa matumaini ya kiroho na kimwili.
Alisema nchi inahitaji uongozi utakaotambua umuhimu wa vijana hasa katika suala la ajira ili kuondoa matatizo mbalimbali yakiwamo ya Panya Road ambayo yameanza kutokea.
“Taifa lipo katika hatari, limegawanyika tumeona katika Bunge Maalumu la Katiba, kuna Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) na Tanzania Kwanza, tunahitaji uongozi utakaotambua haya kwa lengo la kuondoa changamoto hizi ili taifa letu lisiangamie kama mataifa mengine.
“Nawaomba vijana wasikubali kununuliwa na mtu yeyote kwa ajili ya jambo fulani, bali wafanye jambo ambalo wataona linamanufaa kwa taifa letu,” alisema Askofu Mokiwa.
JANUARY MAKAMBA
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amewataka Watanzania kuwaepuka watu wanaotumia fedha nyingi kutafuta uongozi kutokana na kile alichosema, wakifanikiwa kuupata hawatatawala kwa haki.
Alisema taifa likipata kiongozo wa aina hiyo, hataweza kuhukumu kwa haki na pia anaweza kuigawa nchi na watu wake.
Kauli hiyo aliitoa juzi katika sherehe za maulidi kitaifa za kulizaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), zilizofanyika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambapo aliwataka viongozi wa dini nchini wasichoke kuliombea taifa ili amani iliyopo iweze kudumu.
January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, ni mmoja wa makada wa CCM ambao wametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
“Kubwa zaidi msichoke kuombea nchi yetu ipate viongozi wazuri, watakaotenda na kutawala kwa haki, viongozi watakaohukumu kwa haki, viongozi wenye busara, viongozi watakaotuunganisha si watakaotugawanya.
“Ukiona kiongozi anataka kununua uongozi kwa fedha nyingi ni dalili mojawapo kwamba hatatawala kwa haki… ndugu zangu mnaoniskiliza ni muhimu sana tuwakatae wale wanaotaka kulazimisha kupata uongozi kwa kutumia fedha na rushwa.
“… Wale wanaotumia lugha za kuwagawa watu kwa kusema ‘mimi nataka niongoze kwa sababu kundi la watu wangu wananiunga mkono, niko tayari kuwaacha wale waende wanyewe, lakini nichaguliwe na watu wangu’. Watu wa namna hiyo tusiwaruhusu,” alisema January aliyekuwa mgeni mwalikwa katika sherehe hizo.
Alisema mwaka huu, ni muhimu kutokana na nchi kuingia katika uchaguzi mkuu na kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwangalifu ili kuepuka mifarakano inayoweza kujitokeza.
“Tusipokuwa waangalifu uchaguzi utaweza kutufarakanisha, uchaguzi ni ushindani na watu wanasemana, wanashambuliana, wananyoosheana vidole.
“Baadhi ya maeneo ambayo yamekubwa na migogoro na vita duniani, chanzo ni uchaguzi ambao haukuendeshwa vizuri, kwa kwa haki na ulitawaliwa na lugha na kauli za ubaguzi.
“Miaka yote nchi yetu imeshinda majaribu na migawanyiko hii, mwaka 1995, 2000, 2005 na hasa zaidi uchaguzi wa mwaka 2010.
“Katika uchaguzi unaokuja ni jaribio jingine la amani ya nchi yetu. Ni namna gani tunalishinda hili jaribio, amani na umoja wetu ni kukumbuka na urithi wa waasisi wa taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume, walituachia urithi wa taifa moja la watu wanaopendana na wanaoshirikiana,” alisema.
Akizungumzia Katiba mpya, January aliwataka Watanzania kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 30.
“Tutapiga kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, lakini kabla hatujafika huko ni lazima tujiandikishe Februari, nawasihi sote tushiriki kwa kuanza kujiandikisha na baadae tupige kura ya kuweza kupata Katiba itakayotuongoza kwa miaka 20, 30,50 ijayo,” alisema .
Hata hivyo, alisifu kazi kubwa inayofanywa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ya kuongoza Waislamu kwa miaka mingi, ingawa bado taasisi hiyo inahitaji msaada kwa waumini wake waliojaliwa uwezo kiuchumi.
“Taasisi hii, ina uwezo mkubwa Mufti tupo tayari kukusadia ili iwe imara na kuweza kufanya kazi kwa uwezo mkubwa na kuleta heshima kwa jamii,” alisema.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika sherehe hizo, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Bin Simba aliwataka Waislamu kushikamana ili kuhakikisha wanaimarisha uchumi wa waislamu kuanzia ngazi ya msikiti na mtaa, badala ya kutegemea BAKWATA makao makuu pekee.
“Tunapenda suala la kujitegemea tumekuwa ni watu tunaotaka tufanyiwe msikiti tujengewe madrasa tujengewe na hata juzuu tununuliwe. Tumezidi kuomba masheikh
“Watoto ni wetu, tunataka watu watusomeshee leo hii tuna yatima wengi nilianza kuorodhesha yatima 160 kwa Dar es Salam pekee, bado miji mingine je hawa watasomeshwa na nani, tulianzisha mfuko wa maendeleo ambao lengo lake ni kusaidia elimu, lakini hivi sasa hata masheikh kwenye msikiti hawauzungumzi tena,” alisema Mufti Simba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles