24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kijana apigwa kisu baada ya kufumaniwa,

Asifiwe George na Mwajabu Kusupa (TEC), Dar es Salaam
HEKAHEKA za sikukuu ya mwaka mpya wa 2015 jijini Dar es Salaam zimeacha alama ya matukio kadhaa mbali na taarifa za watu 87 kujeruhiwa kwa ajali wakati wa mkesha, pia yapo matukio mengine mawili likiwemo la kijana wa miaka 18 kuuawa baada ya kufumaniwa.
Kabla ya taarifa hizi mpya juzi gazeti la MTANZANIA liliripoti juu ya kutokea kwa ajali katika maeneo tofauti tofauti zilizosababisha watu 87 kujeruhiwa wakiwa katika harakati za kusherehekea mwaka mpya.
Katika tukio la sasa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alisema ingawa matukio katika mkoa wake yamepungua ukilinganisha na sikukuu za aina hiyo kwa miaka mingine, lakini kuna tukio moja la kifo lililoigusa jamii.
Alisema mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam, Hamis Selemani (18), alifariki dunia kwa kuchomwa kisu kifuani baada ya kufumaniwa akifanya mapenzi na binti wa miaka 15.
Kamanda Nzuki alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia mwaka mpya ambapo kijana aliyetambulika kwa jina la Ally Kimodo, alimfumania Selemani akiwa na binti huyo.
Alisema baada ya kuwafumania aliwauliza kulikoni, Kimodo hakuwa na maneno mengi na alichukua jukumu la kumchoma Selemani kisu na hatimaye alitoroka, pia binti huyo ambaye ni mkazi wa Tabata baada ya kuona mchumba wake amechomwa kisu naye pia alitoroka.
Kamanda Nzuki alisema juhudi za kuwatafuta watuhumiwa hao wawili bado zinaendelea ili kuweza kujua ukweli wa tukio hilo.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya, alisema wananchi walisherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu lakini saa 1:30 jioni katika eneo la Paradise Beach Kigamboni, ilikutwa maiti ya mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 ambaye hakutambulika jina lake.
“Mwili huo ulioonekana katika eneo hilo, unaonyesha kuwa marehemu hakufariki dunia sehemu hiyo bali alikuwa akiogelea katika fukwe ya jirani na mwili wake ulikokotwa na maji na kutupwa pembezoni mwa eneo hilo.
“Tunaomba watu ambao hawamuoni ndugu yao watoe taarifa polisi ili waweze kumtambua ndugu yao kwasababu mwili wake tumeuhifadhi katika Hospitali ya Vijibweni,” alisema Kihenya.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alisema hali ya usalama ilitawala katika mkoa wake kwani watu walisherehekea sikukuu kwa amani na hakuna tatizo lolote la uvunjifu wa amani ambalo lilijitokeza.
“Tulikuwa tumeelekeza nguvu nyingi sehemu zenye ibada pamoja na mikusanyiko ya watu wengi lengo lilikuwa ni kulinda usalama kwa wananchi ili waweze kusherehekea sikukuu kwa amani,” alisema Wambura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles