24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Panda shuka ya michezo ndani ya mwaka mmoja wa Magufuli

magu

Na ZAINAB IDDY

NI mwaka mmoja sasa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli aingie madarakani katika awamu ya tano.

Rais Dk. Magufuli aliapishwa rasmi na kuanza majukumu yake ya kuliongoza taifa Novemba 5, 2015 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Watanzania wengi wakishuhudia tukio hilo.

Kwa sasa ametimiza mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani huku akizigusa sekta za uchumi, elimu, kilimo na michezo katika utendaji wake wa kazi.

Tangu Serikali mpya ichukue madaraka, kuna mambo mbalimbali tumeyashuhudia kwenye sekta mbalimbali, huku baadhi ya watendaji wakitumbuliwa na sekta ya michezo nayo ikiwa ni mojawapo iliyoguswa.

Bajeti ya michezo 2016/17

Katika mwaka huu wa fedha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, bajeti imepunguzwa kwa asilimia 21, ukilinganisha na mwaka uliopita wa fedha.

Katika mwaka wa fedha 2015/16, wizara hiyo iliyopo chini ya Waziri Nape Nnauye, iliidhinisha Sh bilioni 21.957 kwa matumizi ya kawaida, lakini mwaka huu wa fedha ulioanza Julai zimetengwa Sh bilioni 17.326, ikiwa ni punguzo la Sh bilioni 4.631 sawa na asilimia 21 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha uliopita.

BMT yatumbuliwa

Katika harakati za kuziboresha sekta ya michezo nchini, Februari 19 mwaka huu, Waziri Nape, alitengua uteuzi wa Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya.

Uamuzi huo ni baada ya kuwasimamisha kazi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo na msaidizi wake, Juliana Yasoda.

Waziri Nape alifikia uamuzi huo wa kumtoa Lihaya kutokana na kukaa kwenye wadhifa huo kwa muda mrefu, bila kuonekana maendeleo ya kueleweka huku akiteuliwa, Mohammed Kiganja, kukaimu nafasi hiyo mpaka atakapoteuliwa katibu mpya.

Umitashumta na Umisseta

Juni 13 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, alitangaza kusitisha mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Nchini (Umitashumta na Umisseta), ambayo ilipangwa kufanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Juni 13 hadi Julai 5 mwaka huu.

Sababu ya kufanya hivyo ilikuwa kupisha zoezi la kumalizia ukamilishaji wa madawati ili kutimiza agizo la Rais Dk. Magufuli la kuondoa upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Mfumo wa ukodishwaji na hisa

Klabu za Simba na Yanga nazo zilijikuta katika mgogoro na Serikali baada ya kutaka kuingia kwenye mfumo wa uendeshaji na uwekezaji wa klabu zao.

Sakata hilo lilianza baada ya klabu hizo kuamua kutoka kwenye umiliki wa timu wa wanachama kuelekea kwenye umiliki wa hisa na ukodishwaji.

Katika suala hilo, Mwenyekiti wa Yanga, alitaka kuikodisha timu hiyo kwa miaka 10, akiimiliki nembo na timu Yanga, wakati kwa upande wa Simba mfanyabiashara, Mohamed Dewji (Mo), akitaka kuchukua hisa asilimia 51 ya kumiliki klabu hiyo.

Wakati wanachama wakibariki mabadiliko hayo ya mfumo wa uendeshaji na Yanga ikiwa tayari imeingia mkataba wa miaka 10 wa ukodishwaji na Kampuni ya Yanga Yetu Limited, Septemba mwaka huu, Simba ikiwa katika hatua ya mwisho kumkabidhi klabu hiyo Mo kwa umiliki wa hisa za asilimia 51.

Serikali kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, alitoa uamuzi wa kusimamisha michakato hiyo hadi timu hizo zitakapofanya mabadiliko ya katiba zao.

Alisema iwapo kama Yanga na Simba zinahitaji kubadili mifumo ya uendeshaji wa klabu zao, ni lazima zifanye marekebisho ya katiba zao kwa mujibu wa Sheria ya Baraza hilo na Kanuni za Msajili namba 442 Kanuni 11 kifungu kidogo cha (1-9).

Kufungwa Uwanja wa Taifa

Katika hali inayoonyesha Serikali imekerwa na vitendo vya uharibifu wa mali zake, Oktoba mbili mwaka huu iliamua kuzizuia timu za Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni baada ya kufanyika kwa uharibifu wa miundombinu ya uwanja huo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kati ya timu hizo Oktoba mosi mwaka huu na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mkono wa TRA waigusa TFF

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wilaya ya Ilala, ilizuia fedha zote kwenye akaunti za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa madai ya shirikisho hilo kuwa na malimbikizo ya kodi ya Sh bilioni1.6.

TRA ilikuwa ikidai asilimia kubwa ya malimbikizo ya kodi hizo yatokanayo na makato ya mshahara (P.A.Y.E) ya makocha wa kigeni wa timu za taifa katika kipindi cha mwaka 2010-2013, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen.

Pia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mchezo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Brazil uliofanyika mwaka 2010, ulichangia deni hilo la kodi kwa asilimia kubwa.

Simbu aweka rekodi Olimpiki

Kwa mara ya kwanza katika historia ya michezo ya Olimpiki tangu mwaka 1980, baada ya Suleiman Nyambui na Filbert Bayi kufanya vizuri nchini Moscow, mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Simbu, aliweka rekodi baada ya kushika nafasi ya tano kwenye mbio za marathon za kilomita 42, Agosti 21 mwaka huu mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Kujengwa uwanja mkubwa Dodoma

Miongoni mwa mambo yaliyowafariji wanamichezo wengi nchini ni baada ya Mfalme wa Morocco, Mohammed VI, kuahidi kujenga uwanja wa kisasa wa michezo mkoani Dodoma.

Rais Dk. Magufuli alimwomba mfalme huyo alipotembelea Tanzania hivi karibuni kwa ziara ya siku tano.

Ombi hilo la Rais Dk. Magufuli lilikubaliwa na mfalme huyo ambaye aliahidi kuijenga uwanja huo utakaogharimu dola milioni 80 hadi 100, sawa na Sh bilioni 171.216.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles