23.5 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Simulizi ya Akothee, aisee acha kabisa!

akothee

Na BADI MCHOMOLO

SAFARI ya maisha ya nyota wa muziki nchini Kenya, Esther Akoth ‘Akothee’ ni ndefu na yenye visa vingi. Huyu ni msanii anayefanya vizuri kwa sasa na anatamba na wimbo wake wa ‘Sweet Love’ ambao amemshirikisha Mbongo Fleva, Nasib Abdul ‘Diamond’.

Hapa chini ni baadhi ya mambo ambayo inawezekana ulikuwa huyajui kutoka kwa msanii huyo ambaye manunuzi ya baadhi ya vitu vyake hufanya Ulaya; ana magari ya  thamani na nyumba nne za kisasa mjini Mombasa, Pwani ya Kaskazini, Nairobi na Rakwaro.

 

ALIOLEWA AKIWA NA MIAKA 14

Akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia yao, alipewa kila kitu huku wazazi wake wakitamani kumuona akifika mbali hasa katika elimu na yeye mwenyewe alipenda maisha ya kujiachia.

Mama wa Akothee alikuwa ni mwanasiasa wakati baba wa mrembo huyo alijihusisha na masuala ya utawala.

Mrembo huyo anadai kuwa baada ya kupelekwa katika Shule ya Wasichana ya Nyabisawa, hapo alikutana na kijana ambaye alikuwa anasoma katika shule ya wavulana ambayo ilikuwa karibu na shule hiyo ya wasichana.

“Ukweli ni kwamba kijana huyo alinifanya niyaelewe mapenzi kuliko hata shule maana nilijiona kama nimechanganyikiwa.

“Kutokana na hali hiyo tuliamua kukimbia shule na kuishi pamoja, wazazi wangu walitaka nirudi shule lakini nilikataa na kuamua kuolewa nikiwa na miaka 14 tu,” anasema.

 

Alikuwa dada wa kazi kwa miaka saba

Baada ya kuacha shule na kuamua kuolewa, alijikuta akiishi maisha magumu, hivyo aliamua kuhangaika kwa ajili ya kutafuta kazi.

Alijikuta akipata kazi ya ndani (House Girl) kwa miaka saba. Mwenyewe anasema: “Niliamua kufanya kazi za ndani kwa mama wa mume wangu kwa miaka saba huku mume wangu akiwa shule anaendelea na masomo na nilifanikiwa kupata mtoto nikiwa kwa mama yake.”

 

Miaka 16, watoto watatu

Msanii huyo alipata mtoto mara baada ya kuacha shule akiwa na umri wa miaka 14, baada ya hapo kila mwaka alipata mtoto tangu alipofikisha miaka 14, 15 na 16.

 

Auza dagaa mitaani

Baada ya kuondoka ukweni, msanii huyo alizidi kuwa na maisha magumu ambapo alikwenda kuishi Kanga, hivyo aliamua kuingia sokoni na kufanya biashara ya kuuza dagaa maarufu kwa jina la ‘Omena’.

Mwaka 2003, mume wake alimaliza chuo, akaamua kukaa na familia yake huku Akothee akiamua kurudi shule.

“Niliamua kurudi shule kwa ajili ya kumaliza elimu ya Sekondari katika Shule ya Kanyasrega, huku watoto wangu wakianza shule ya watoto, jioni nilikuwa nakwenda kuwachukua shule na kuwapeleka nyumbani huku nikiendelea kuuza Omena kwa saa moja,” anasema.

 

Amwagana na mpenzi wake

Inasemekana kwamba mwaka huo mume wa Akothee alianza kupata fedha kutokana na elimu aliyoipata, hivyo alipata mchumba mwingine na kuamua kuachana na Akothee.

“Nadhani sikuwa mrembo kwake kwa kipindi hicho, hivyo aliamua kuniacha, nikiwa na watoto watatu,” anaendelea kusimulia.

 

Awa dereva taksi

“Kuna wakati nilijiona kama paka kila kitu nikikishika kwa mikono yote, nikaamua kufanya kazi ya udereva taksi  mjini Mombasa.”

Akiwa katika kazi hiyo alipata bahati ya kukutana na raia wa Switzerland, ambapo alitaka kujua kwa nini anafanya kazi kama hiyo kwa mrembo wake.

Mazungumzo yao yaliwafanya waingie kwenye uhusiano na baadaye kumchukua hadi nchini Switzerland, lakini inasemekana kuwa jamaa huyo alikuwa na lengo la kuzaa naye na siyo kufunga ndoa.

Kutokana na hali hiyo Akothee aliamua kurudi nchini Kenya na kuanza kufanya muziki. Aliweza kufanya muziki na kujipatia kipato cha kutosha ambacho kilimwezesha kuendesha maisha yake na kununua magari kwa ajili ya kazi ya taksi.

“Itakuwa ngumu kuwa na mwanaume kwa sasa ni bora nikae na watoto wangu, mwanaume gani ambaye atakubali nimzalie watoto huku mimi mwenyewe nina watoto watano, nani atakubali?

“Miezi michache iliyopita nilipoteza watoto wawili mapacha, hivyo ni bora kwa sasa niendelee na muziki na kuangalia familia yangu,” anasema Akothee.

Maoni/ushauri 0714107464

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles