Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Msanii maarufu wa muziki wa Hip Hop kutoka Marekani, Sean Combs, anayejulikana zaidi kama P Diddy, anakabiliwa na tuhuma nzito za unyanyasaji wa kingono kutoka kwa watu wapya 120, wakiwemo wanaume 60 na wanawake 60.
Kwa mujibu wa mawakili wanaowakilisha waathiriwa, baadhi ya matukio hayo yanadaiwa kutokea wakati waathiriwa walipokuwa watoto, huku mmoja akidai kuwa alinyanyaswa akiwa na umri wa miaka tisa.
Tuhuma hizo zinadaiwa kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka huu wa 2024, zikigusa kipindi kirefu cha takriban miongo mitatu. Tony Buzbee, ambaye ni wakili wa waathiriwa, amesema kuwa anatarajia kufungua kesi ndani ya mwezi mmoja ujao, huku sehemu kubwa ya mashtaka hayo yakitarajiwa kufikishwa mahakamani katika majimbo ya New York na Los Angeles.
Kwa upande mwingine, P Diddy tayari anakabiliwa na kesi nyingine zinazohusiana na usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara ya ngono, ambapo amekanusha vikali mashtaka hayo, akiyaita ya uongo na njama za kumchafua jina. Wakili wake ameendelea kusisitiza kuwa msanii huyo, ambaye pia ni baba wa watoto saba, atathibitisha kutokuwa na hatia mahakamani.
Tangu Septemba 17, 2024, P Diddy amekuwa kizuizini baada ya kukana mashtaka ya kumlazimisha wanawake kushiriki vitendo vya kingono wakiwa wamelewa, pamoja na mashtaka mengine ya ulanguzi wa wanawake wanaojiuza na njama za ulaghai. Wakili wake ameomba dhamana ya dola milioni 50 ili Diddy awekwe chini ya uangalizi wa kifaa cha GPS akiwa nyumbani kwake Florida, lakini ombi hilo limekataliwa hadi sasa.
P Diddy, ambaye alianzisha lebo ya Bad Boy Records mwaka 1993, ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa kwenye tasnia ya muziki wa Hip Hop na amejijengea jina kubwa kwa muda mrefu. Kesi hii inachochea taharuki kubwa kwenye tasnia ya muziki na kuacha mashabiki na wadau wakisubiri kwa hamu kuona jinsi mambo yatakavyokwenda mahakamani.