27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

OSHA yapongezwa kwa utendaji unaoridhisha

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imeeleza kuridhishwa kwake na maboresho yaliyofanywa na Taasisi mbali mbali zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-(Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kuwahudumia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kauli hiyo ya Kamati imetolewa leo na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, mara baada ya kuhitimisha kikao cha kamati hiyo kilichopokea na kujadili taarifa kuhusu miundo na majukumu ya Taaasisi mbali mbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mchengerwa amesema katika vikao hivyo wamekutana na wizara mbali mbali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) pamoja na Taasisi zake.

“Tumekuwa na mfululizo wa vikao vya kamati na tumekutana na Wizara na Taasisi mbali mbali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kujadili muundo na majukumu ya ofisi hiyo. Kupitia taarifa zilizowasilishwa tumejionea namna ambavyo utendaji umeboreka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka mitano iliyopita (2015-2020) hivyo tunaipongeza Wizara na Taasisi zake kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanyika,” amesema Mchengerwa.

Aidha, Mchengerwa amefafanua kuwa kwasasa Taasisi nyingi zimejiimarisha ambapo alitolea mfano Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na kueleza kuwa ni Taasisi ambayo imefanya kazi kubwa katika kuimarisha masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi hapa nchini kupitia uboreshaji wa mifumo yake ya utendaji.

Kwa mujibu wa Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji amesema walitumia kikao hicho kuweka mipango na mikakati ya kuendelea kuzishauri Taasisi wanazozisimamia namna bora zaidi ya kuendelea kuboresha utendaji wake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Ulemavu), Jenista Mhagama, akifafanua jambo katika kikao cha Kamati ya Katiba na
Sheria ambapo Taasisi chini ya Wizara yake ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na
majukumu yao.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Wizara inayoshughulikia Masuala ya Kazi chini ya Waziri, Jenista Mhagama pamoja Taasisi husika ambazo ni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kufanya mageuzi makubwa katika mifumo na taratibu zake kiutendaji ambayo yamepelekea kuboresha huduma kwa wananchi.

“Leo tumepata mada nzuri sana kutoka kwa menejimenti ya OSHA kwasababu sote tunakwenda kazini ambako athari mbali mbali zitokanazo na mazingira ya kazi ambayo si rafiki zinaweza kutokea hivyo kupitia maelezo hayo tumeona njinsi ambavyo OSHA imejipanga kulinda nguvu kazi ya Taifa letu,” amesema Asha Abdallah Juma ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa upande wake, Yahaya Massare, Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na Mbunge wa Manyoni Magharibi amesema hatua ya OSHA kufuta baadhi ya tozo zake ambazo zilionekana kuwa kero kwa wamiliki wengi wa sehemu za kazi, imepelekea mwitikio mkubwa wa wadau katika kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu ya Taasisi yake mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria.

Vikao hivyo vya Kamati mbali mbali za kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo vilianza kufanyika tangu Januari 18, 2021, vinafanyika muda mfupi kabla ya kuanza rasmi kwa vikao vya Bunge la 11 ambavyo vinatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Februari 2, 2021 jijini Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles