23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mwongozo utoaji chanjo za mifugo wazinduliwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amezindua mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini ili kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika utoaji chanjo na kulinda afya ya mnyama.

Hivi karibuni waziri huyo aliagiza kusimamishwa kwa muda utoaji wa chanjo unaofanywa na halmashauri nchini kupitia kampuni walizoingia nazo mikataba baada ya kubaini chanjo kutolewa kiholela kwa mifugo bila kuwepo utaratibu sahihi na kusababisha madhara kwa mifugo na hasara kwa mfugaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mukunda, mwongozo wa utoaji chanjo dhidi ya magonjwa nchini kati ya sekta binafsi na umma baada ya kuuzindua jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul.

Waziri Ndaki amesema katika kuhakikisha mwongozo huo unakuwa na tija kwa taifa, ametaka kuwepo kwa haki na wajibu kwa wadau wote wa mifugo ili kuelewa vyema haki na wajibu huo katika kusimamia mwongozo huo na kufikia matokeo chanya katika kuboresha afya ya mifugo.

“Mambo ya msingi kabisa kwenye jambo hili ni afya ya mifugo, afya ya mifugo ilikuwa hatarini ni kweli utaratibu wanafanya halmashauri lakini hauko wazi sana, ndiyo maana tukasema sasa ni muhimu kuwa na mwongozo huu kutuelekeza nini cha kufanya, chanjo ikifanywa vizuri kwa usahihi bila makosa tuliyokuwa tunayaona tunaweza kuwa na ng’ombe wenye afya bora na njema,” amesema Waziri Ndaki.

Aidha amesema mwongozo huo ambao umeshirikisha wadau zaidi ya 30 wakati wa kuuandaa na kwamba wizara ipo tayari kupokea maoni ya wadau sehemu ambazo utaonekana kuwa na mapungufu ili kuurekebisha na kuufanya uwe bora zaidi, lengo likiwa ni kuhakikisha afya ya mifugo nchini inalindwa na mfugaji kutopata hasara ya mifugo yake kufa au kupata madhara mengine yoyote baada ya kuchanjwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini, Jeremiah Wambura, mwongozo wa utoaji chanjo dhidi ya magonjwa nchini kati ya sekta binafsi na umma baada ya kuuzindua jijini Dodoma.

Katika kuhakikisha kuwa serikali inaendeleza mahusiano mazuri na sekta binafsi, Waziri Ndaki amesema wizara itahakikisha inaandaa mazingira mazuri ya kuwa pamoja na sekta binafsi ili kufanya kazi pamoja ambayo itakuwa na tija kwa taifa na wafugaji kwa ujumla.

“Sekta binafsi nipende kuwahakikishia kwamba sisi tutafanya kazi na sekta binafsi vizuri kabisa tusiwe na mashaka ni vile tuliona kasoro, lakini niwaombe sekta binafsi hasa wale mlio vizuri katika jambo hili la chanjo msiwe na wasiwasi hata mkiingia mikataba na halmashauri ili mradi muwe na sifa na vigezo ndiyo maana ya sisi tukatoa mwongozo ili tufanye kazi pamoja,” amesema.

Pia amewataka viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mamlaka za serikali za mitaa, watoa huduma za afya ya mifugo na sekretarieti za mikoa wazingatie maelekezo yaliyopo kwenye mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini na kutoa maoni au kuuliza maswali sehemu ambazo zitakuwa na utata ili kuhakikisha unatekelezwa kama ambavyo umezingatiwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini.

Waziri huyo ameagiza kutolewa nakala za kutosha za mwongozo huo kwa wadau wa sekta ya mifugo kote nchini huku pia akiwataka wadau kupata nakala laini kupitia tovuti ya wizara hiyo www.mifugouvuvi.go.tz.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mukunda, amesema mkoa huo utahakikisha yale yote ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatamani yatokee katika sekta ya mifugo watayasimamia ili yalete tija kwa taifa na wafugaji na kuiomba wizara kuangalia ikama ya wataalamu wa afya ya mifugo na pia wale waliopo katika ngazi za juu kuwa na utaratibu wa kufika katika maeneo ya chini ya wafugaji.

“Ili mwongozo huu uweze kufanya vizuri ikama ya wataalamu wa mifugo bado haitoshi hivyo, ni vyema wataalamu waliopo katika ngazi za juu waweze kuwafikia pia wafugaji wa chini na tunataka kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kitovu cha kuzalisha nyama na maziwa kwa wingi,” amesema Mukunda.

Amesema sekta ya mifugo kwa sasa imekuwa ikirasimishwa rasmi na kuifanya iheshimishe watu wanaofanya shughuli za mifugo kwa kuwa imekuwa na tija kubwa kwa taifa na mtu mmoja mmoja.

Katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul, amesema serikali bado inafanya jitihada mbalimbali za kupata masoko zaidi ya mazao ya mifugo yenye ubora ambayo yanachochewa na uwepo wa chanjo bora na mifugo kupatiwa chanjo hiyo kwa njia sahihi na pia kutoa angalizo kwa halmashauri nchini kuhakikisha zinakuwa na miundombinu bora kwa ajili ya kuogeshea mifugo.

“Wenzangu niwaombe huu waraka ukatusaidie ili malalamiko ya mnada umeharibika au wilaya nzima kutokuwa na josho yafike mwisho, kupitia mapato mbalimbali ambayo halmashauri wamekuwa wakipata yakiwemo ya minada iliyopo kwenye wilaya hizo wanapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kuyakarabati,” amesema Gekul.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini, Jeremiah Wambura, amesema tasnia ya maziwa ikisimamiwa vyema inaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa pato la taifa na kuhamasisha uwepo wa viwanda vingi vya kuchakata maziwa nchini.

Ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia vyema namna ya kuisimamia tasnia ya maziwa ili iwe na tija zaidi kwa taifa pamoja na kuongeza wingi wa maziwa ambayo yanaweza kutumika majumbani pamoja na kuchakatwa viwandani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles