25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

OPRAH WINFREY ALIVYOLIZA WANAWAKE TUZO ZA GOLDEN GLOBES

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO


JANUARI 7, ulikuwa usiku wa staa wa vipindi vya runinga pamoja na filamu, Oprah Winfrey, baada ya kutwaa tuzo ya Golden Globes.

Licha ya kujawa na furaha kubwa kwa kutwaa tuzo hiyo, lakini wanawake wengi waliosikiliza hotuba ya mwanaharakati huyo walijikuta wakitokwa na machozi kila walipoendelea kuisikiliza hotuba hiyo.

Tuzo hizo za awamu ya 75 kutolewa tangu kuanzishwa kwake, zinatolewa kwa watu wanaotoa mchango mkubwa katika ulimwengu wa burudani.

Hata hivyo, tuzo hizo ni mara ya kwanza kutolewa tangu prodyuza wa filamu na runinga, Harvey Weinstein, atuhumiwe kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa wasanii zaidi ya 80.

Wengi walichukia kitendo hicho cha unyanyasaji kwa watoto wa kike, hivyo tuzo hizo zilisimama kwa muda hadi pale hatua za kisheria zilipochukuliwa.

Kutokana na hali hiyo mtandao wa MeToo na Time Up, uliandaa mjadala wa mpango wa kupambana na unyanyasaji uliodhaminiwa na wanawake wenye nguvu kubwa kwenye filamu nchini Marekani (Hollywood).

Baadhi ya wasanii walioonyesha kujitoa kwa moyo wao mmoja ni pamoja na Oprah Winfrey, Natalie Portman na wengine wengi.

Mjadala huo ulichangia kwa kiasi kikubwa Oprah kuingia kwenye tuzo hizo na kufanikiwa kuchukua na kuwa mwanamke wa kwanza rangi nyeusi kuweza kuichukua tuzo hiyo.

Kuna baadhi ya sababu zilizomfanya Oprah aweze kuweka historia ya kuwa mwanamke mweusi wa kwanza kuchukua tuzo hiyo.

Usawa

Mara nyingi Oprah katika vipindi vyake amekuwa akiwapigania wanawake kwa kiasi kikubwa ili waweze kujikomboa katika maisha yao, hivyo amekuwa akipenda usawa kati ya wanaume na wanawake ili kuwapa wanawake nafasi ya kufanya jambo lolote ambalo mwanaume anaweza kulifanya.

Oprah anatajwa kuwa na utajiri wenye thamani ya dola bilioni 2.8 kwa mujibu wa mtandao wa Forbes, hivyo amekuwa akiamini kwamba wanawake wana uwezo wa kufanya kila kitu endapo watapewa nafasi.

Huruma

Katika mjadala huo ambao ulifanywa na Time Up, mrembo huyo alionesha huruma yake kwa wanawake wote duniani hasa waliofanyiwa unyanyasaji wa kijinsia, hivyo hakuweza  kuzungumzia wale walionyanyaswa na Harvey Weinstein.

Imani ya Oprah ni kwamba wapo wanawake wengi wanaonyanyaswa kwenye mambo mbalimbali duniani, hivyo anajitahidi kupaza sauti yake duniani kote kupitia vitabu pamoja na vipindi mbalimbali vya runinga ili kupinga vikali unyanyasaji.

Msimamo

Oprah aliweka wazi kuwa tangu ameanza kufanya kazi kwenye runinga na filamu, amekuwa na misimamo yake ambayo ilikuwa ikimpa imani ya kufikia malengo yake licha ya kukutana na changamoto mbalimbali.

Mambo hayo matatu ndiyo yaliyompa nafasi kubwa Oprah kuingizwa kwenye tuzo hizo kwa mara ya kwanza na kuchukua.

Baada ya kutwaa tuzo hiyo alitoa hotuba iliyowagusa wengi kiasi kwamba wakatokwa na machozi, hotuba iliyowalenga wasichana wenye umri mdogo wenye fikra ya kufanya mambo makubwa.

“Siku mpya ipo kwenye upeo wa macho, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wanawake wote waliovumilia miaka ya unyanyasaji nawaona kama mama zangu, walikuwa na ndoto ya kufanya makubwa lakini hawakufanikiwa kutokana na kukatishwa tamaa ya unyanyasaji.

“Napenda kutumia nafasi hii kwa ajili ya kuwapa nguvu wasichana wenye malengo makubwa na bado hawajayafikia, kikubwa wanatakiwa kuweka wazi kile ambacho kipo kwenye vichwa vyao hata kama kuna unyanyasaji.

“Wanawake tumekuwa hatuaminiwi kama tunaweza kupaza sauti mbele ya wanaume na kufanya jambo kubwa duniani, niweke wazi kuwa huu ndio wakati wa mwanamke kufanya makubwa.

“Kwa wale wasichana wanaofuatilia hotuba hii nataka kuwaambia kwamba, siku mpya ipo kwenye upeo wenu, wakati siku hiyo mpya itakapoanza itakuwa kwa sababu ya wanawake wengi, wanawake hao wakiamua kuitumia siku hiyo kwa kujituma kwa bidii wanaweza kuwa viongozi.

Tuzo hiyo ya Golden Globe, pia ilipewa jina la Cecil B. DeMille kutokana na nyota huyo wa filamu kuwa na mchango mkubwa kwenye soko la burudani la Hollywood. Cecil B. DeMille alifanikiwa kupewa tuzo hiyo ya heshima Februari 21, 1952. Baada ya hapo tuzo hiyo ikapewa jina la Golden Globe.

Mwanamke wa kwanza kuchukua tuzo hiyo alikuwa Judy Garland, mwaka  1962, akiwa na umri wa miaka 39 na kuwa mwanamke wa kwanza kuchukua tuzo hiyo akiwa na umri mdogo, lakini Sidney Portier alikuwa mwanaume wa kwanza rangi nyeusi kufanikiwa kutwaa tuzo hiyo mwaka 1982 na sasa ni Oprah Winfrey.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles