29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

OPEC kupandisha bei ya mafuta Tanzania?

 Waziri wa mafuta wa Iran, Bijan Zanganeh
Waziri wa mafuta wa Iran, Bijan Zanganeh

NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM

UAMUZI wa mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) kupunguza uzalishaji wa mafuta, umezua sintofahamu kuhusu bei ya bidhaa hiyo.

Uamuzi huo wa OPEC ambao unaelezwa kuwa ni wa kwanza kuchukuliwa katika kipindi cha miaka minane, tayari umesababisha bei ya mafuta ghafi duniani kupanda kwa karibu asilimia sita.

Wakizungumzia uamuzi huo wa OPEC, wadau wa sekta ya nishati hiyo wamesema athari ya punguzo hilo inategemeana na soko na kwamba kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ni vigumu kutabiri matokeo yake kwa sasa.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo, akizungumza na MTANZANIA Jumamosi alisema athari ya uamuzi huo wa OPEC kwa Tanzania itachukua muda kuonekana.

“Inategemea, unajua hatuwezi kutabiri yajayo, inawezekana bei ikapanda ama ikawa ile ile kwa hiyo suala la kushuka au kupanda inategemea siwezi kusema lolote kwa sasa,” alisema.

Wanachama wa OPEC wamekuwa wakilaumiana kusababisha mdororo wa bei ya mafuta kutokana na kushindwa kuwa na msimamo wa pamoja wa kudhibiti bei.

Katika uamuzi huo wa OPEC, uzalishaji wa mafuta utapunguzwa hadi mapipa 700,000 kwa siku, ingawa upunguzaji wa uzalishaji hautakuwa sawa miongoni mwa nchi wanachama.

Akichangia maamuzi hayo, Waziri wa mafuta wa Iran, Bijan Zanganeh, alisema amepokea uamuzi huo kwa mikono miwili.

Zanganeh alisema OPEC imechukua uamuzi wa kipekee huku taarifa zikisema Iran itaruhusiwa kuongeza uzalishaji wake.

Baada ya tangazo hilo kutolewa mafuta ghafi ya Brent yanayotumiwa kama kigezo cha mafuta kimataifa yalipanda bei na kufikia karibu asilimia 6 hadi Dola za Kimarekani 49 kwa kila pipa.

Mawaziri wa mafuta wa nchi wanachama wamesema maelezo ya kina kuhusu mwafaka wa sasa yatajadiliwa katika mkutano mwingine utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Awali kulikuwa na sintofahamu baina ya Iran na mpinzani wake Mashariki ya Kati Saudi Arabia, jambo ambalo lilikuwa limezuia kupatikana kwa mwafaka.

Wazalishaji wadogo wa mafuta walipigania kupunguzwa kwa uzalishaji baada ya mafuta kushuka bei kutoka Dola za Kimarekani 110 miaka miwili iliyopita.

Nigeria ambayo ni moja ya Taifa lililoathirika na bei hiyo, Waziri wake wa mafuta, Ibe Kachikwu, alipongeza uamuzi wa sasa wa OPEC akisema ni mzuri sana.

Waziri wa Nishati wa Algeria, Noureddine Bouarfaa, amesema uamuzi huo ulifikiwa kwa kauli moja.

Waziri wa Nishati wa Qatar, Mohammed Bin Saleh Al-Sada ambaye ndiye rais wa sasa wa OPEC, amesema uzalishaji sasa utakuwa kati ya mapipa milioni 33.2 na milioni 33 kwa siku.

Nayo ripoti ya Benki ya Dunia ‘Africa’s  Pulse’ inayotolewa mara mbili kila mwaka, imesema uchumi umetikisika hasa kwa wafanyabiashara wa mafuta.

Ikaongeza kuwa wakati baadhi ya nchi barani Afrika zikidorora kiuchumi, nchi kama Tanzania, Rwanda, Ethiopia, zimekua kiuchumi kwa asilimia zaidi ya 6 ambapo Ivory Coast na Senegal zimeshika nafasi za juu kiuchumi.

“Ripoti hii imechambua ni kwa jinsi gani  nchi ambazo uchumi wake umeendelea kuwa imara kwa kuwa na sera nzuri za kiuchumi, mazingira bora na taratibu bora za kisheria katika biashara, kukua kwa mauzo nchi za nje,” amesema Mchumi Mkuu wa Benki ya dunia kwa nchi za Afrika, Akbert Zeufack, kwenye ripoti hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles